39. Majina bandia ya wazushi kwa Ahl-us-Sunnah

Ni katika hekima ya Allaah (Ta´ala) kumjaalia kila Mtume kukabiliwa na madui katika wahalifu. Wanazuia kutokamana na haki kiasi na wanavyoweza kwa maneno na vitendo. Wanafanya hivo kwa vitimbi, utata na propaganda mbalimbali. Allaah anafanya hivo ili haki iweze kubainika, kuwa wazi na kuishinda batili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake walikutana na mambo kama haya mara nyingi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَتَسْمَعُنَّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُواْ الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ وَمِنَ الَّذِينَ أَشْرَكُواْ أَذًى كَثِيرً

“Bila shaka mtasikia kutoka kwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu na kutoka kwa wale walioshirikisha udhia mwingi.”[1]

Wale washirikina madhalimu walimpa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake majina mengi bandia. Waliwaita kuwa ni washirikina, wendawazimu, makuhani, waongo na mengineyo.

Ilipokuwa kwamba wanachuoni na waumini ndio warithi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), walikabiliwa na wanafalsafa na wazushi kama mfano wa yale yaliyomkabili Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake kutoka kwa wale washirikina. Kila kundi likawa linawapa jina la bandia Ahl-us-Sunnah kwa mambo ambayo Allaah amewatakasa nayo. Walisema hivo ima kwa sababu ya ujinga wao wa kutoijua haki kwa vile walidhania wako katika haki na kwamba Ahl-us-Sunnah ndio wako upotofuni, au kwa sababu ya makusudio mabaya kwa vile wanataka kuwakimbiza watu na Ahl-us-Sunnah na kufanya ushabiki juu ya maoni yao pamoja na kujua kuwa wako makosani.

Jahmiyyah na Mu´attwilah wengine wanawaita Ah-us-Sunnah “Mushabbihah”. Wanadai eti endapo mtu atamthibitishia sifa Allaah basi amemshabihisha na viumbe.

Raafidhwah wamewaita Ahl-us-Sunnah kuwa ni “Nawaaswib” kwa kuwa wanampenda Abu Bakr na ´Umar kama wanavyowapenda watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanadai kuwa yule mwenye kumpenda Abu Bakr na ´Umar basi amewachukia watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndio maana wanasema:

“Hakuna kupenda bila kuchukia.”

Bi maana mtu hawezi kuwapenda watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa mpaka kwanza amchukie Abu Bakr na ´Umar.

Qadariyyah wanawaita Ahl-us-Sunnah kuwa ni “Jabriyyah”. Kwa sababu wanaona kuwa kuamini Qadar ina maana ya kutenzwa nguvu.

Murji-ah wanawaita Ahl-us-Sunnah, wenye kufanya uvuaji katika imani, kwamba ni “wenye mashaka”. Murji-ah wanasema kuwa imani ni kuthibitisha kwa moyo peke yake. Hivyo mwenye kufanya uvuaji katika imani anaitilia shaka imani yake kwa mtazamo wa hawa Murji-ah.

Wanafalsafa na watu wa mantiki wanawaita Ahl-us-Sunnah kuwa ni “Hashwiyyah”, ikiwa na maana kwamba hawana kheri yoyote. Vilevile wanawaita kuwa ni “magugu” kwa vile hakuna kheri yoyote ndani yake. Vivyo hivyo wanawaita kuwa ni “taka la povu” kwa sababu ya ule uchafu inaobeba. Wanamantiki hawa wanaonelea kuwa asiyefahamu mantiki, hawi na uhakika juu ya jambo lake. Wanaonelea kuwa mtu huyo mmoja miongoni mwa wale ambao hakuna kheri yoyote ndani yao. Uhakika wa mambo ni kwamba elimu hii ambayo wao wanajifakhirisha kwayo haifidishi kitu juu ya haki. Shaykh (Rahimahu Allaah) amesema katika “ar-Radd ´alaa al-Mantwiqiyyiyn”:

“Mimi daima hutambua kuwa mantiki ya kigiriki mwerevu haihitajii kama ambavyo vilevile haiwezi kumnufaisha yule mpumbavu.”[2]

[1] 03:186

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (3/52)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 89-90
  • Imechapishwa: 13/05/2020