39. Hukumu ya uasi dhidi ya mtawala wa Kiislamu

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yule anayefanya uasi dhidi ya kiongozi wa waislamu ambaye watu wamekusanyika juu yake na wakakubali ukhaliyfah wake kwa njia yoyote ile, kwa kuridhia au kwa nguvu, amewatawanyisha waislamu na ameenda kinyume na mapokezi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mfanya uasi huyu akifa katika hali hii, basi amekufa kifo cha kipindi cha kikafiri.”

MAELEZO

Haijuzu kumfanyia uasi kiongozi wa waislamu ijapokuwa atakuwa ni mtenda maasi na madhambi. Kuna sampuli mbili za uasi:

1- Uasi wa kimatendo na mapambano.

2- Uasi wa kimaneno, uchokozi na uchochezi. ´Ubaadah bin as-Swaamitw (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituita kuja kula kiapo ambapo tukampa kiapo cha kusikiliza na kutii kwa kupenda kwetu na kutokupenda kwetu, katika kipindi chepesi na kigumu, pindi mtu anapopendelewa juu yetu na kwamba tusivutane na watawala mpaka pale mtakapoona ukafiri wa wazi ambao tuna dalili kwao kutoka kwa Allaah.”[1]

Kuna Hadiyth nyingi na zenye kutambulika katika maudhui haya. Miongoni mwazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayefanya uasi dhidi ya mtawala akafa, basi amekufa kifo cha kipindi cha kikafiri.”[2]

Kama tulivosema kuna Hadiyth nyingi na zenye kutambulika katika maudhui haya.

Ni uasi pia kule kutaja mabaya ya kiongozi, kuwatukana, kuwakemea mbele ya umati wa watu na kuwatweza. Mambo kama haya yanapelekea katika khatari kubwa na madhara makubwa ikiwa ni pamoja vilevile na watawala kuasiwa na yanapelekea katika uasi wa kimatendo. Uasi wa kimatendo unapelekea kumwagika kwa damu, heshima kuvunjwa, njia kufungwa na kutandaa kwa khofu.

Enyi wanafunzi! Mcheni Allaah juu ya Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)! Msihadaike na watu wenye mirengo ya kisiasa. Nchi yetu[3] ni ya Kiislamu. Inatilia umuhimu suala la Tawhiyd, inahukumu kwa Shari´ah ya Allaah na inaeneza uadilifu. Tunamuomba Allaah aiongoze mahakama yake katika kila kheri. Hatusemi kwamba haina makosa. Hapana shaka kwamba makosa yapo, lakini makosa haya yanatakiwa kurekebishwa kwa njia yenye manufaa na si yenye madhara, kama mfano wa nasaha za siri na mfano wa hayo.

Sipendi kuingia ndani zaidi katika mlango huu. Ni ishara tu tunazoashiria na kulenga juu ya makosa ya watu wa Bid´ah. Huenda Allaah akamwongoza kwazo na akatulinda na shari za Bid´ah na watu wa Bid´ah – kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa na mkarimu.

[1] al-Bukhaariy (7056) na Muslim (1709).

[2] al-Bukhaariy (7053) na Muslim (1849).

[3] Saudi Arabia – Allaah aikinge na kila ovu.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 143-144
  • Imechapishwa: 30/04/2019