Kuhiji kwenda katika Nyumba tukufu ya Allaah kila mwaka ni wajibu wa kutosheleza juu ya Ummah wa Kiislamu. Ni wajibu kwa kila muislamu ambaye ametimiza masharti ya kuhiji kwenda kuhiji japo mara moja katika umri. Yatayozidi hapo imependekezwa. Hajj ni moja katika nguzo za Uislamu. Hajj ni fungu la mwanamke wa Kiislamu kutokamana na Jihaad kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Ee Mtume wa Allaah! Je, mwanamke ana Jihaad?” Akasema: “Ndio, wana Jihaad isiyokuwa na mapigano; Hajj na ´Umrah.”

Ameipokea Ahmad, Ibn Maajah na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.

al-Bukhaariy amepokea kutoka kwake ya kwamba amesema:

“Ee Mtume wa Allaah! Tunaona kuwa Jihaad ndio kitendo bora zaidi. Si tupambane?” Akasema: “Lakini Jihaad bora ni hajj yenye kukubaliwa.”

Katika hajj kuna hukumu ambazo ni maalum kwa mwanamke ikiwa ni pamoja na:

1 – Mahram. Hajj ina masharti yenye kuenea kwa mwanaume na mwanamke: Uislamu, akili, uungwana, kubaleghe na uwezo wa kimali. Mwanamke ana sharti maalum ambayo ni kumpata Mahram wa kusafiri pamoja naye kwenda hajj. Mtu huyo anaweza kuwa baba yake au ambaye ameharamika kwake maharamisho ya milele kwa nasabu kama mfano wa baba, mtoto wake au kaka yake. Au kwa sababu iliyohalali kama mfano wa kaka yake waliyenyonya ziwa moja, baba yake wa kambo au mtoto wa kiume wa mume wake. Dalili ya hayo ni yale aliyopokea Ibn ´Abbas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kuwa amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitoa Khutbah na akasema:

“Mwanaume asikae faragha na mwanamke isipokuwa awe pamoja naye Mahram na wala asisafiri mwanamke isipokuwa awe pamoja naye Mahram. Mwanaume mmoja akasimama akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mke wangu ametoka kwenda kuhiji na mimi nimeandikwa kwenye vita kadhaa na kadhaa.” Akasema: “Nenda uhiji na mke wako.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke asisafiri isipokuwa awe pamoja naye Mahram.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Hadiyth juu ya haya ni nyingi ambazo zinamkataza mwanamke kusafiri kwenda kuhiji na kwenginepo bila ya kuwa na Mahram. Kwa sababu mwanamke ni dhaifu na hufikwa na vipingamizi na shida mbalimbali safarini ambazo hakuna awezaye kuyakabili isipokuwa wanaume. Jengine ni kwamba anakuwa ni tamanio la mafusaki. Kwa hiyo ni lazima awepo Mahram awezaye kumkinga na kumuhami kutokamana na maudhi yao.

Ni sharti kwa Mahram huyu ambaye ataandamana na mwanamke katika hajj yake awe na akili, amekwishabaleghe na muislamu. Kafiri haaminiwi juu yake. Akikata tamaa ya kupata Mahram basi atalazimika kumteua mtu wa kumuhijia.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 83-84
  • Imechapishwa: 07/11/2019