39. Hadiyth ya Jibriyl kuhusu Uislamu, Imani na Ihsaan

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili kutoka katika Sunnah ni Hadiyth ya Jibriyl inayojulikana iliyopokelewa na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Siku moja tulipokuwa tumekaa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutokea mtu ambaye nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana. Hakuwa na alama ya kuonesha kuwa ni msafiri na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua. Alienda akakaa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaweka magoti yake karibu na mago yake na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake.” Akasema: “Ee Muhammad, nieleze kuhusu Uislamu!” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Uislamu ni kushuhudia kuwa hapana mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha Swalah, kutoa Zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji ukiweza.” Akasema: “Umesema kweli.” Tukashangazwa kwa kumuuliza kwake Mtume na kumsadikisha. Kisha akasema: “Nieleze kuhusu imani!” Akasema: “Ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake na siku ya Mwisho na kuamini Qadar; kheri na shari yake.” Akasema: “Umesema kweli!” Akasema: “Nielezee kuhusu Ihsaan!” Akasema: “Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye Anakuona.” Akasema: “Nieleze kuhusu Qiyaamah.” Akasema: “Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile muulizaji.” Akasema: “Nieleze kuhusu alama zake!” Akasema: “Kijakazi kumzaa bibi yake na utaona wachunga wanaenda miguu chini, uchi na mafukara wakishindana kujenga majumba marefu.” Amesema: “Kisha akaondoka na tukatulia muda mrefu. Halafu akasema (Swallla Allaahu ´alayhi wa salalm): “Ee ‘Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza?” Nikajibu: “Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.” Akasema Mtume: “Ilikuwa ni Jibriyl ambaye amekuja kuwafundisha Dini yenu.”

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 45
  • Imechapishwa: 26/01/2017