Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya shauku, woga na unyenyekeaji ni maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ

“Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri na walikuwa wakituomba kwa matumaini na khofu na walikuwa Kwetu wenye kunyenyekea.” (al-Anbiyaa´ 21 : 90)

MAELEZO

Shauku (Raghbah) ni mapenzi ili mtu aweze kulifikia jambo linalopendwa.

Woga (Rahbah) ni khofu inayomzalishia mtu kumkimbia yule anayeogopwa. Nayo inahusiana na khofu iliyoambatana na kitendo.

Unyenyekeaji (Khushuu´) ni udhalilifu na unyonge kwa utukufu wa Allaah kwa njia ya mtu kujisalimisha na hukumu Zake za ulimwengu na za Kishari´ah.

Katika Aayah hii tukufu Allaah (Ta´ala) amewasifu waja Wake wa kweli ya kwamba wanamuomba Allaah (Ta´ala) kwa shauku, woga pamoja na kumyenyenyekea. Katika maana hii imekusanya du´aa ya ´ibaadah na du´aa ya maombi. Wanamuomba Allaah ilihali wakiwa na shauku kwa yale alionayo  na thawabu Zake, pamoja na kuogopa adhabu Zake na athari ya madhambi yake. Muumini katika juhudi zake kwa Allaah (Ta´ala) anatakiwa kuwa baina ya khofu na matarajio. Matarajio yawe na nguvu kipindi cha wakati wa ´ibaadah, ili apate uchangamfu na kutaraji yakubaliwe, khofu yake iwe na nguvu zaidi endapo atapotaka kufanya maasi ili aweze kukimbia yale maasi na kuokoka na adhabu yake.

Baadhi ya wanachuoni wamesema upande wa matarajio uwe na nguvu zaidi katika hali ya ugonjwa na khofu iwe na nguvu zaidi katika hali ya afya njema. Kwani mgonjwa ni mdhaifu na huenda kifo chake kiko karibu na akafa hali ya kuwa ni mwenye kumdhania vyema Allaah (´Azza wa Jall). Na katika hali ya uzima, anakuwa ni mchangamfu na anatarajia kubaki maisha marefu. Kwa ajili hiyo hilo linamfanya kutenda madhambi na kuwa na kiburi. Kwa hivyo upande wa khofu unatakiwa kuwa na nguvu zaidi ili aweze kusalimika kutokamana na hilo.

Vilevile imesemekana kwamba matarajio na khofu yawe katika ngazi moja ili matarajio yasimpelekei akahisi kusalimika na adhabu ya Allaah, kama jinsi khofu pia isimfanye akakata tamaa na rehema za Allaah. Yote mawili ni sifa mbaya zinazomwangamizi mwenye nazo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 25/05/2020