1 – Mwanamke mwenye istihaadhah: Ni yule anayepata damu ambayo si hedhi, kama tulivyotangulia kusema. Ni lazima kwake kufunga na wala haijuzu kwake kula kwa sababu ya damu hii ya ugonjwa. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa” wakati alipotaja kuhusu kula kwa mwenye hedhi:

“Tofauti na mwanamke mwenye damu ya ugonjwa. Damu ya ugonjwa inaenea nyakati za zama na haina wakati anapoamrishwa mwanamke kufunga na ikawa hilo haliwezekani kujilinda nayo kama vile kushindwa na matapishi, kutokwa na damu kwenye donda, majipu, kuota na mfano wa hayo ambayo hayana wakati maalum ambapo mtu anaweza kujiepusha nayo. Kwa hiyo hilo halikufanywa kupingana na swawm kama ilivyo juu ya damu ya hedhi.”

2 – Ni wajibu kwa mwanamke mwenye hedhi, mjamzito na mnyonyeshaji pindi wanapokula walipe kati ya Ramadhaan moja waliyokula na Ramadhaan inayofuatia. Kuharakisha ndio bora zaidi. Kusipobaki juu ya Ramadhaan inayofuata isipokuwa kiasi cha masiku ambayo alikula basi ni lazima kwao kulipa funga zao ili wasiingiliwe na Ramadhaan nyingine. Vilevile ni lazima kwao kufunga Ramadhaan iliokabla yao. Wasipofanya hivo na wakaingiliwa na Ramadhaan na bado wanadaiwa masiku ya Ramadhaan iliyopita – na wakati huohuo hawana udhuru wa kuchelewesha – basi itawalazimu kulipa na kulisha masikini kwa kila siku moja iliyowapita. Ikiwa walichelewesha kwa udhuru basi hakuna kinachowalazimu zaidi ya kulipa. Vivyo hivyo yule ambaye anawajibika kulipa kwa sababu ya kuacha kwake kufunga kutokana na maradhi au safari basi hukumu zao ni kama hukumu ya ambaye ameacha kufunga kwa sababu ya hedhi kutokana na upambanuzi uliyotangulia.

3 –  Haijuzu kwa mwanamke kufunga swawm ya sunnah ikiwa mume wake hayuko safarini isipokuwa kwa idhini yake mume. al-Bukhaariy, Muslim na wengineo wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si halali kwa mwanamke kufunga na mume wake yuko isipokuwa kwa idhini yake.”

Katika baadhi ya mapokezi kwa Ahmad na Abu Daawuud imekuja:

“… isipokuwa Ramadhaan.”

Ama mume wake akimruhusu kufunga swawm za sunnah, awe mbali na yeye au mwanamke huyo hana mume, basi imependekezwa kwake kufunga swawm za sunnah na khaswakhaswa masiku ambayo imependekezwa kwake kufunga kama vile siku ya jumatatu na alkhamisi, siku tatu kila mwezi, siku sita za Shawwaal, siku kumi za Dhul-Hijjah, siku ya ´Arafah, siku ya ´Aashuuraa´ na siku nyingine kabla yake au baada yake. Isipokuwa haitakikani kwake kufunga swawm ya sunnah ilihali anadaiwa masiku ya Ramadhaan mpaka kwanza alipe madeni yake. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

4 – Mwanamke mwenye hedhi akitwahirika katikati ya mchana wa Ramadhaan basi atatakiwa kujizuia mchana uliyobaki na kuilipa siku hiyo pamoja na yale masiku aliyokula kwa sababu ya hedhi. Ni lazima kwake kujizuia mchana uliyobaki kwa sababu ya kuuheshimu wakati.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 88-89
  • Imechapishwa: 07/11/2019