38. Shubuha ya pili ya watu wa Tawassul na majibu juu yake

2- Shubuha ya pili: Wanafanya wakatikati baina yao na baina ya Allaah kwa ajili ya kumuadhimisha Allaah. Wanasema kwamba Allaah ni Mkubwa na wala hafikiwi isipokuwa kwa mkatikati na waombezi ambao watakuombea Kwake na kukukalia kati. Wanadai namna hii ya kuwa ni katika kumuadhimisha Allaah kwa njia ya kwamba hafikiwi isipokuwa kwa ukatikati. Kama jinsi wafalme wa duniani hawafikiwi isipokuwa mpaka kupatikane wakatikati na waombezi. Kutokana na madai yao kumepatikana yafuatayo:

Jambo la kwanza: Wamemlinganisha Allaah (Jalla wa ´Alaa) na wafalme wa duniani, jambo ambalo ni la batili. Huku sio kumuadhimisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Bali kinyume chake ni kumtia upungufu Allaah kwa kule kufanya kwao kitu katika aina za ´ibaadah kumfanyia mwingine. Shirki ni kumfanya Allaah kuwa na upungufu. Sio kumuadhimisha, kama wanavodai wao.

Jambo la pili: Kumlinganisha Allaah na viumbe, huku pia ni kumtia mapungufu Allaah. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anazijua hali za waja Wake. Lakini watu na wafalme hawazijui haja za raia wao isipokuwa mpaka kupatikane mtu mwenye kuwafikishia haja za raia wao. Kwa sababu wao ni watu. Ama Allaah (Jalla wa ´Alaa) anajua na wala hahitajii wa kumfikishia haja za waja Wake.

Jambo la tatu: Wafalme wa duniani wanalazimika kukubali maombezi ya waombezi kwa sabuabu anawahitajia wasaidizi na mawaziri. Iwapo atawakatalia maombi yao watamkaripia na kumfanyia uadui. Kwa hiyo wanayakubali maombezi yao ijapokuwa watakuwa ni wenye kuyachukia hayo ili waweze kubakia katika ufalme wao na watu wawapende. Lakini Allaah (Jalla wa ´Alaa) Yeye amejitosheleza kutokamana na waja Wake. Hahitajii mawaziri na waombezi kama wafalme wa duniani ambapo wanalazimika kukubali maombezi yao hata kama hawakuridhia, kama walivyo wafalme wa duniani. Wafalme wa duniani wanalazimika kukubali maombezi ya mawaziri na wengineo. Ama Allaah (Jalla wa ´Alaa) Yeye Amejitosheleza kutokaman na waja Wake.

Jambo la nne: Wafalme wa duniani – mara nyingi – hawataki kutoa kheri wala hawatoi waliotakwa isipokuwa kwa kung´ang´aniwa. Ama Allaah (Jalla wa ´Alaa) Yeye ni mkarimu na wala haathirwi na yeyote kama wanavyoathiriwa wafalme wa duniani. Allaah unapomuomba, basi Yeye yukaribu na ni Mwenye kujibu. Hahitajii mkatikati. Tofauti na wafalme wa duniani. Wao hawatoi waliotakwa na kuombwa isipokuwa baada ya usumbufu mkubwa, kama inavyojulikana. Kwa kuwa wao ni watu. Sifa ya mwanadamu ni ugumu na ubakhili. Ama Allaah (Jalla wa ´Alaa) Yeye yukaribu na ni Mwenye kujibu, yukaribu na ni tajiri (Subhaanahu wa Ta´ala).

Jambo la tano: Wafalme wa duniani ni mafukara. Vinaisha vile wanavyomiliki. Wakati mwingine huenda wakaishiwa na wakahitajia kukopwa na kuwaibia wengine. Ama Allaah (Jalla wa ´Alaa) Yeye ndiye Mwenye kuzimiliki hazina za mbinguni na ardhini. Yeye ni tajiri na mkarimu. Haja za viumbe wote Kwake ni kama alivosema katika Hadiyth ya kiungu:

“Enyi waja Wangu! Ingelikuwa wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu, binaadamu katika nyinyi na majini katika nyinyi mkasimama sehemu pamoja na mkaniomba na Nikawapa kila mmoja alichoomba, haitonipunguzia katika nilicho Nacho zaidi kuliko sindano inavyopunguza bahari inapochovywa.”[1]

Lau viumbe, kuanzia wale wa mwanzo mpaka wa mwisho wao, watasimama sehemu moja na kila mmoja akamuomba Allaah mahitajio yake na Allaah akawapa mahitajio yao yote, basi hayo hayatopunguza chochote katika ufalme Wake. Hilo ni tofauti na wafalme wa duniani. Wakitoa vile walivyonavyo vinaisha. Amesema (Ta´ala):

مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ بَاقٍ

“Mlivyo navyo nyinyi vinatoweka na vilivyoko kwa Allaah ni vya kubakia.” (an-Nahl 16: 96)

Kwa hiyo kumlinganisha Muumba (Subhaanah) na viumbe kwa kumfanyia wakati na kati ni ulinganisho batili kwa njia nyingi.

[1] Ameipokea Muslim (2577) kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 63-65
  • Imechapishwa: 09/08/2018