38. Ni ipi hukumu ya ambaye amepangusa juu ya soksi za ngozi baada ya kumalizika kwa muda uliowekwa wa kupangusa na akaswali kwazo?

Swali 38: Ni ipi hukumu ya ambaye amepangusa juu ya soksi za ngozi baada ya kumalizika kwa muda uliowekwa wa kupangusa na akaswali kwazo?

Jibu: Ukimalizika muda wa kupangusa katika soksi za ngozi na mtu akaswali baada ya kumalizika kwa muda, basi analazimika kutawadha upya, kuosha miguu yake na kuirudi swalah yake. Kwa vile hakuosha miguu yake ameswali akiwa na wudhuu´ usiyokuwa kamilifu.

Ama ukimalizika muda uliowekwa wa kupangusa lakini mtu bado akingali na twahara na akaswali baada ya kumalizika kwa muda wa kupangusa, swalah yake ni sahihi kwa sababu kumalizika kwa muda wa kupangusa hakuchengui wudhuu´. Hata kama baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa kumalizika kwa muda wa kupangusa kunachengua wudhuu´, lakini haya ni maoni yasiyokuwa na dalili. Kutokana na haya ukimalizika muda wa kupangusa lakini bado mtu yuko na twahara yake (ijapo ni baada ya siku nzima) basi inafaa kwake kuswali. Wudhuu´ wake umethibiti kwa mujibu wa dalili ya ki-Shari´ah na hivyo haichenguki isipokuwa kwa mujibu wa dalili ya ki-Shari´ah. Isitoshe hakuna dalili kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inayojulisha kwamba kumalizika kwa muda uliowekwa wa kupangusa unawajibisha kutawadha na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/180)
  • Imechapishwa: 06/05/2021