38. Mwenye busara na hasadi II


1 – Hakuna njia ambayo ni salama zaidi kumwepuka hasidi isipokuwa kujiweka mbali naye. Muda wa kuwa bado anaona neema zako basi hilo halitomzidishia jengine isipokuwa kujihisi vibaya na kumjengea dhana mbaya Allaah na hasadi yake itazidi kukua.

2 – Mwenye busara anahakikisha anaua hasadi yake kwa kiasi anachoweza. Hakuna kinachopingana na hasadi kama kujiweka mbali na hasidi. Hasidi hakuhusudu kwa sababu ya kasoro ulionayo au usaliti uliojitokeza kwako. Anakuhusudu kwa sababu ya kutoridhia hukumu na mipango ya Allaah.

3 – Hammaad bin Humayd alisema kumwambia al-Hasan al-Baswriy:

“Ee Abu Sa´iyd! Hivi muumini anakuwa na hasadi?” Akajibu: “Ni wingi ulioje kusahau kwako wakati wana wa Ya´quub walivomuhusudu Yuusuf. Ficha hasadi kifuani mwako. Haitokudhuru kitu muda wa kuwa hujaitamka wala kufanya kitu.”

4 – Mwenye busara akiingiwa akilini mwake na jambo la kumuhusudu ndugu yake basi hupambana kuficha hasadi yake na kuacha kuonyesha yale alionayo.

5 – Mara nyingi hasadi inakuwa kwa wale watu wa ngazi moja au waliokaribana kingazi. Hakuna mtu anayefikia ngazi yoyote ya dunia hii isipokuwa atakuweko mtu anayemchukia au kumuhusudu kwayo.

6 – Hasidi ni muhasimu mkaidi. Haitakikani kwa mwenye busara kumwacha hasidi akahukumu endapo kutatokea jambo. Akihukumu, basi atahukumu kwa hasara ya mpinzani wake. Akikusudia jambo, basi atalikusudia kwa hasara ya mpinzani wake. Akizuia, basi hatozuia isipokuwa kwa hasara ya mpinzani wake. Akipeana, basi atawapa wengine na si mpinzani wake. Hakuna jengine kilchofanywa na mpinzani wake isipokuwa zile neema ambazo hasidi anazihusudu. Kwa hivyo mtu atahadhari na watu wenye sifa zilizotajwa hapo juu. Wanaweza kuwa watu mfano wake, marafiki zake, majirani zake na mabinamu zake.

7 – al-´Abbaas bin Bakkaar amesema:

“Kuna bwana mmoja alisema kumwambia Shubayb bin Shabbah: “Hakika mimi nakupenda.” Shubayb akasema: “Najua.” Akasema: “Umejuaje?” Akajibu: “Kwa sababu sio jirani wala binamu yangu.”

8 – Ni alama mbaya iliyoje ya hasadi. Hasadi inarithisha huzuni na majonzi na ni ugonjwa usiyokuwa na dawa.

9 – Hasidi anapoona neema kwa ndugu yake hunyamaza. Anapoona kosa kwa ndugu yake basi hufurahi. Uso wake unajulisha kile kilichomo moyoni mwake. Sijwahi kumuona hasidi akimsalimisha yeyote.

10 – Hasadi inaita katika taabu. Humuoni Ibliys? Alimuhusudu Aadam na hivyo hasadi yake ikawa ni taabu moyoni mwake. Matokeo yake akawa ni mwenye kulaaniwa baada ya kuwa ni mwenye kunyanyuliwa juu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 135-137
  • Imechapishwa: 06/08/2021