38. Mambo ya kuzingatia wakati wa kumuosha maiti II

11- Kitavuliwa katika yale yaliyotajwa katika “jambo la nne” Muhrim. Haijuzu kumpaka manukato. Hayo ni kutokana na maneno yake katika Hadiyth ambayo nimetangulia kuishiria punde kidogo:

“Msimpake mafuta ya maiti.

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Wala msimtie manukato. Kwani hakika atafufuliwa siku ya Qiyaamah akiwa ni mwenye kuleta Talbiyah.”

Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengineo kama ilivyotangulia katika ukurasa wa 22-23.

12- Kunavuliwa vilevile katika yale yaliyopokelewa katika “jambo la tisa” wanandoa. Inajuzu kwa kila mmoja wao kusimamia jambo la kumuosha mwengine. Kwani hakuna dalili inayolikataza. Isitoshe msingi ni kufaa na khaswa kwa kuzingatia kwamba ni jambo linatiwa nguvu na Hadiyth mbili:

Ya kwanza: ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Lau ningeliamua kuliendea jambo langu basi nisingelirudi nyuma; asingelioshwa isipokuwa na wake zake.”

al-Bayhaqiy amesema:

“Akaonesha huzuni zake juu ya hilo. Haifai kuhuzunika isipokuwa kwa kitu kinachojuzu.”

Kujuzu ndio maoni ya Imaam Ahmad, kama alivyopokea Abu Daawuud katika “Masaa-ilih”.

Ameipokea Ibn Maajah. Abu Daawuud na wengine wamepokea kutoka kwake mwishoni mwa Hadiyth ambayo imetangulia punde kidogo kuhusu kumuosha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ya pili: ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza tena:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alirejea kwangu kutoka katika jeneza huko al-Baqiy´ na mimi nilikuwa nahisi maumivu kichwani mwangu na nikisema na huku nikisema: “Ee kichwa changu!” Akasema: “Bali mimi ndiye “ee kichwa changu”; ni kipi kitachokudhuru endapo utakufa kabla yangu nikakuosha, nikakuvisha sanda halafu nikakuswalia na kukuzika.”

Ameipokea Ahmad (06/228), ad-Daarimiy (01/37-38), Ibn Maajah (01/448), Abu Ya´laa katika “al-Musnad” (4579), Ibn Hishaam katika “as-Siyrah” (02/336), ad-Daaraqutwniy (192) na al-Bayhaqiy (03/396). Ndani yake yumo Muhammad bin Ishaaq ambaye ni mudalisi na ameitaja kwa mtindo wa “kutoka kwa fulani, kutoka kwa fulani”. Isipokuwa katika upokezi wa Abu Ya´laa na Ibn Hishaam ambapo amehadithia kwa kuweka wazi – na himdi zote anastahiki Allaah. Ingawa al-Haafidhw Ibn Hajar ametaja katika “at-Talkhiysw” (02/107) ya kwamba amefuatwa na Swaalih bin Kaysaan kwa Ahmad na an-Nasaa´iy.

Iko kwa Ahmad (06/144). Lakini hakukutajwa waziwazi jambo la kuosha. Mtu arejee upokezi wa an-Nasaa´iy pengine ndani yake ametaja jambo hilo. Mimi sikuiona Hadiyth hiyo katika kitabu chake “Sunan as-Sughrah”. Pengine ipo katika kitabu chake “Sunan al-Kubraa”.

Kisha nikaiona katika “Tuhfati al-Ashraaf” (11/482) limetajwa kwa uchache “kufa” katika “Sunan al-Kubraa”.

13- Wasimamie kumuosha wale ambao ni wajuzi zaidi kuhusu Sunnah ya uoshaji na khaswa wakiwa ni katika familia na ndugu zake. Kwa sababu wale waliosimamia kumuosha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa kama tulivyotaja. ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nilimuosha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nikawa natazama yale yanayokuwa kwa maiti na sikuona chochote na alikuwa mzuri akiwa hai na akiwa mfu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ameipokea Ibn Maajah (01/447), al-Haakim (01/362), al-Bayhaqiy (03/388) na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh, kama alivosema katika “az-Zawaaid” (q. 01/92). al-Haakim amesema:

“Ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.”

adh-Dhahabiy amemkosoa kwa kusema:

“Ndani yake kuna mkato.”

Haya ni miongoni mwa mambo yasiyokuwa na hoja. Kwani Hadiyth ni katika mapokezi ya Ma´mar, kutoka kwa az-Zuhriy, kutoka kwa Sa´iyd bin Musayyib kutoka kwa ´Aliy. Cheni hii imeungana na ni yenye kutambulika baadhi wamepokea kutoka kwa wengine. Ma´mar kupokea kutoka kwa az-Zuhriy na az-Zuhriy kupokea kutoka kwa Sa´iyd ni jambo limetangaa zaidi na halihitajii kutajwa. Sa´iyd kupokea kutoka kwa ´Aliy  kumeungana vilevile, kama ambavyo al-Haafidhw alivyoashiria hilo katika “at-Tahdhiyb”. Bali ameonelea kuwa amesikia kutoka kwa ´Umar pia[1].

Katika “al-Mursal” ya ash-Sha´biy imetajwa kwamba ´Aliy pamoja na al-Fadhwl –  bi maana Ibn ´Abbaas – ndio waliomuosha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Usaamah bin Zayd.

Ameipokea Abu Daawuud (02/69) na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh Mursal.

Ipo Hadiyth nyingine inayoitolea ushahidi kutoka katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas.

Ameipokea Ahmad (3358) kwa cheni ya wapokezi dhaifu.

[1] Kuhusu aliyoyataja juu ya ´Umar ni jambo linahitaji kutazamwa vizuri. Hivi sasa mimi sina nafasi ya kulibainisha. Kuhusu kusikia kwake kutoka kwa ´Aliy ni jambo la kweli. Hilo ni kwa sababu kifo cha  ´Aliy kilikuwa katika mwaka wa arubaini. Kipindi hicho Sa´iyd alikuwa na umri wa miaka ishirini na nane. Kukatika basi kuko wapi?

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 66-69
  • Imechapishwa: 17/02/2020