al-Jabbaar – Bi maana Allaah (Jalla wa ´Alaa). Moja katika majina Yake ni al-Jabbaar. al-Jabbaar lina maana nyingi:

1 – Ambaye wanawaunga na kuwatia moyo waja Wake waliovunjika moyo.

2 – Ambaye hukumu Zake za kimakadirio zinapita kwa waja Wake bila ya wao kupingana nazo. Hukumu Zake (Jalla wa ´Alaa) za kimakadirio hazirudishwi.

3 – Maana yake nyingine ya kilugha ni Aliye juu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) yuko juu ya viumbe Wake:

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ

“Naye ni mshindi Aliye juu ya waja Wake, Naye ni Mwenye hekima, Mjuzi wa kila kitu.” (06:18)

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۖ وَيُرْسِلُ عَلَيْكُمْ حَفَظَةً

“Naye ni mshindi Aliye juu ya waja Wake na anakutumieni walinzi.” (06:61)

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… hushuka katika kila usiku.”

Kama ilivyokuja katika Hadiyth.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… pasi na namna… “

Bi maana hatujui namna ya kushuka huko. Hakuna anayejua hili isipokuwa Allaah peke yake. Haimlazimu haya malazimisho yaliyowekwa na wakanushaji, wafananishaji na washabihishaji kwa sababu sisi hatutafiti namna hii. Hakika Allaah juu ya kila kitu ni muweza. Viumbe hawawezi kumzunguka Yeye wote kwa kumtambua. Hakuna anayejua namna ilivyo dhati Yake wala namna yalivyo majina na sifa Zake isipokuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kadhalika al-Jabbaar hushuka jioni ya ´Arafah na hujifakhari kwa waja Wake Malaika na kusema:

“Watazameni waja Wangu wamenijia wakiwa timtimu wamejaa vumbi kutoka katika kila kona ya dunia. Ninakushuhudisheni kwamba hakika Mimi nimewasamehe.”[1]

Hii ni aina nyingine ya kushuka. Mola wetu hushuka jioni ya ´Arafah katika mbingu ya dunia kama ambavyo Anashuka kila usiku katika nyusiku za mwaka pindi kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku. Haya ni kutokana na upole na huruma Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa waja Wake.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… ametukuka… “

Bi maana ametukuka uwezo Wake kufanyiwa namna au kwa sisi kutambua namna yalivyo majina na sifa Zake. Miongoni mwazo ni kushuka. Sisi tunathibitisha kushuka na wala hatupekui namna. Ni kama sifa nyenginezo zote: kushuka kunajulikana. Kuhusu namna haijulikani. Hivyo ndivyo alivyosema Maalik (Rahimahu Allaah) juu ya kulingana ya kwamba:

“Kulingana (Istiwaa´) inajulikana. Namna haijulikani.”[2]

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… Mmoja… “

Mmoja ni katika majina ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hakika Yeye (Subhaanah) ni Mmoja pekee ambaye hana mshirika katika dhati, majina na sifa Zake, matendo na ´ibaadah Zake.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… mwenye kuhimidiwa… “

Mwenye kusifiwa kwa sifa za kusifiwa kamilifu.

[1] Ahmad (02/305), Ibn Hibbaan (3852) na wengineo

[2] Tazama “ar-Radd ´alaa al-Jahmiyyah”, uk. 33 ya ad-Daarimiy na “I´tiqaad Ahl-is-Sunnah” (03/527) (928)  ya al-Laalakaa´iy

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 99-100
  • Imechapishwa: 09/01/2024