38. Maana tatu ya Jabbar


Jabbar – Bi maana Allaah (Jalla wa ´Alaa). Moja katika majina Yake ni Jabbaar. Jabbar lina maana nyingi:

Ya kwanza: Ambaye anawapa moyo waja Wake waliovunjika moyo.

Ya pili: Ambaye hukumu Zake za kimakadirio zinapita kwa waja Wake bila ya wao kuzizuia. Hukumu Zake (Jalla wa ´Alaa) za kimakadirio hazirudishwi.

Ya tatu: Maana yake nyingine ya kilugha ni Aliye juu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) yuko juu ya viumbe Wake:

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ

“Naye ni mshindi Aliye juu ya waja Wake, Naye ni Mwenye hikmah, Mjuzi.” (06:18)

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۖ وَيُرْسِلُ عَلَيْكُمْ حَفَظَةً

“Naye ni mshindi Aliye juu ya waja Wake na anakutumieni walinzi.” (06:61)

hushuka katika kila usiku – Kama ilivyokuja katika Hadiyth.

bila ya namna… – Bi maana hatujui namna ya kushuka huko. Hakuna anayejua hili isipokuwa Allaah peke yake. Haimlazimu haya malazimisho yaliyowekwa na wakanushaji, wafananishaji na washabihishaji kwa sababu sisi hatutafiti namna hii. Hakika Allaah juu ya kila kitu ni muweza. Viumbe hawawezi kumzunguka Yeye wote kwa kumtambua. Hakuna anayejua namna ilivyo dhati Yake wala namna yalivyo majina na sifa Zake isipokuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kadhalika Jabbar hushuka jioni ya ´Arafah na hujifakhari kwa waja Wake Malaika na kusema:

“Watazameni waja Wangu wamenijia wakiwa timtimu wamejaa vumbi kutoka katika kila kona ya dunia. Ninakushuhudisheni kwamba hakika Mimi nimewasamehe.”[1]

Hii ni aina nyingine ya kushuka. Mola wetu hushuka jioni ya ´Arafah katika mbingu ya dunia kama ambavyo Anashuka kila usiku katika nyusiku za mwaka pindi kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku. Haya ni kutokana na upole na huruma Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa waja Wake.

… ametukuka… – Bi maana ametukuka uwezo Wake kuwekewa namna au kwa sisi kutambua namna yalivyo majina na sifa Zake. Miongoni mwazo ni kushuka. Sisi tunathibitisha kushuka na wala hatutafiti namna. Ni kama sifa zingine zote: kushuka kunajulikana. Kuhusu namna haijulikani. Hivyo ndivyo alivyosema Maalik (Rahimahu Allaah) juu ya kulingana ya kwamba:

“Kulingana (Istiwaa´) inajulikana. Namna haijulikani.”[2]

… Mmoja… – Mmoja ni katika majina ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hakika Yeye (Subhaanah) ni Mmoja Peke ambaye hana mshirika katika dhati, majina na sifa Zake, matendo na ´ibaadah Zake.

… mwenye kuhimidiwa… – Mwenye kusifiwa kwa sifa za kusifiwa kamilifu.

[1] Ahmad (02/305), Ibn Hibbaan (3852) na wengineo

[2] Tazama “ar-Radd ´alaa al-Jahmiyyah”, uk. 33 ya ad-Daarimiy na “I´tiqaad Ahl-is-Sunnah” (03/527) (928)  ya al-Laalakaa´iy