228- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema pindi baadhi ya Maswahabah waliposema kuwa wapangilia kuacha kula nyama, kuswali usiku mzima pasi na kulala, kufunga pasi na kula na kutooa:

“Ama mimi nafunga na wakati mwingine sifungi, ninaswali na kulala, ninakula nyama na kuoa wanawake. Mwenye kuipa mgongo Sunnah yangu basi huyo si katika mimi.”[1]

229- Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“´Uthmaan bin Madh´uun alitaka kuishi maisha ya bachala ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkataza. Vinginevyo tusingeliishi maisha ya upekee.”[2]

230- Ndugu! Imekubainikia katika mlango huu na mingine iliyotangulia kwamba kuipa nyongo dunia haina maana ya kuvitenga vya halali na kuharamisha vilivyo vizuri. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ مَنْ حَرَّمَ زِينَةَ اللَّـهِ الَّتِي أَخْرَجَ لِعِبَادِهِ وَالطَّيِّبَاتِ مِنَ الرِّزْقِ ۚ قُلْ هِيَ لِلَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا خَالِصَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ

“Sema: “Nani aliyeharamisha mapambo ya Allaah ambayo amewatolea waja Wake na vizuri katika riziki?” Sema: “Hivyo ni kwa ajili ya wale walioamini katika uhai wa dunia na vitakuwa makhsusi [kwa waumini pekee] siku ya Qiyaamah. Hivyo ndivyo Tunavyofafanua Aayaat kwa watu wanaojua.” (07:32)

يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ

“Enyi Mitume! Kuleni katika vizuri na tendeni mema – hakika Mimi kwa yale myatendayo ni Mjuzi.” (23:51)

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَاجًا وَذُرِّيَّةً ۚ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Kwa yakini Tulituma Mitume kabla yako na tukawajaalia wawe na wake na dhuria. Haiwi kwa Mtume yeyote yule kuleta ishara yoyote isipokuwa kwa idhini ya Allaah.” (13:38)

231- Dini inahusiana na kuwafuata mwongozo wa waja wema katika Maswahabah, Taabi´uun na maimamu wa Salaf.

232- Zayd bin Thaabit ambaye alikuwa ni katika waliobobea zaidi katika elimu alipokea zawadi ya Mu´aawiyah na mtoto wake Yaziyd.

233- Ibn ´Umar, pamoja na uchaji Allaah na fadhila zake, alikuwa akipokea zawadi za shemeji yake al-Mukhtaar bin Abiy ´Ubaydillaah na akila chakula chake. al-Mukhtaar hakuwa mzuri kabisa.

234- Ibn Mas´uud ambaye alikuwa amejaza elimu kuna mtu alimuuliza:

“Mimi nina jirani ambaye anakula ribaa na haepuki pato la haramu. Ananialika nyumbani kwake chakula cha mchana. Niitikie wito?” Ibn Mas´uud akasema: “Ndio. Kala na yeye ndiye mwenye madhambi midhali hujui kwa kulenga ni kipi kilicho cha haramu.”

235- ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) amesema pindi alipoulizwa juu ya zawadi ya mtawala:

“Chinja nyama ya nyumbu.”

236- ash-Sha´biy alikuwa ni katika Taabi´uun wakubwa. Alikuwa ni mwalimu wa mtoto wa ´Abdul-Maalik bin Marwaan na anapokea zawadi zake na kula chakula chake.

237- Ibraahiym an-Nakha´iy na wanachuoni wengine wote Kuufah, al-Hasan al-Baswriy na wanachuoni wengine wote Baswrah, Abu Salamah bin ´Abdir-Rahmaan, Abaan bin ´Uthmaan na wanachuoni sana wa al-Madiynah isipokuwa Sa´iyd bin al-Musayyab walipokea zawadi ya mtawala.

238- az-Zuhriy alipokea zawadi za mtawala ambazo ilikuwa ndio sehemu kubwa ya chumo lake. Hali kadhalika Abuz-Zinaad, Maalik, Abu Yuusuf, ash-Shaafi´iy na wanachuoni wengine wote ´Iraaq na Hijaaz.

239- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kinachokujia pasina wewe kukipupia au kuiomba unatakiwa kuipokea.”

Hapa ndipo mwisho wa kitabu na himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] al-Bukhaariy (5063) na Muslim (1052).

[2] Muslim (1402).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 134-138
  • Imechapishwa: 18/03/2017