38. Asiyeswali amekufuru


Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yule mwenye kuacha swalah amekufuru. Hakuna katika matendo kitu kukiacha ni kufuru isipokuwa swalah. Mwenye kuiacha ni kafiri. Allaah amehalalisha kumuua.”

MAELEZO

Wale wanaomkufurisha asiyeswali wana dalili nyingi na zenye nguvu kabisa juu ya hilo. Upande mwingine wapo ambao hawawakufurishi wale wenye kuacha swalah kwa sababu wanayafasiri maandiko haya. Miongoni mwa dalili za wale wenye kuonelea kuwa asiyeswali ni kafiri ni:

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ

“Wakitubu na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah, basi ni ndugu zenu katika dini.”[1]

Udugu haupatikani isipokuwa baada ya imani, swalah na zakaah:

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَخَلُّوا سَبِيلَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Wakitubu na wakasimamisha swalah na wakatoa Zakaah, basi waacheni huru. Hakika Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[2]

Hawaachwi huru na kuondoshewa upanga isipokuwa mpaka wamuamini Allaah, wasimamishe swalah na watoe zakaah. Ni dalili nyingi sana na zenye nguvu ikiwa ni pamoja vilevile na:

“Ahadi iliyopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Yule mwenye kuiacha basi amekufuru.”[3]

“Kati ya mja na kufuru na shirki ni kuacha swalah.”[4]

Swalah ni kitu kikubwa sana. Swalah ni nguzo ya Uislamu, kama itakavyokuja katika Hadiyth ya ´Abdullaah bin Shaqiyq. Imaam Ahmad ameashiria vivyo hivyo na kusema:

“Hakuna katika matendo kitu kukiacha ni kufuru isipokuwa swalah.”

Katika kijitabu hiki Imaam Ahmad anachagua kumkufurisha asiyeswali. Amtumia hoja maoni yake kwa Hadiyth na kwa maneno ya ´Abdullaah bin Shaqiyq:

“Hakuna kitu Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakionelea kukiacha ni kufuru isipokuwa swalah.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah ametaja namna ambavyo wengi katika wanachuoni katika Maswahabah na wengineo wanamkufurisha yule asiyeswali. Maimamu wengi na wanachuoni wanamkufurisha yule mwenye kuacha moja katika nguzo za Uislamu. Ina maana kwamba yule mwenye kuacha swalah ni kafiri, mwenye kuacha kutoa zakaah ni kafiri, mwenye kuacha kuhiji ni kafiri. Imaam Ahmad ana maoni mengi juu ya Takfiyr kwa yule mwenye kuacha moja katika nguzo hizi. Ana maoni mengine ambayo hamkufurishi isipokuwa tu yule mwenye kuacha kuswali na kutoa zakaah. Katika maoni yake mengine anamkufurisha tu yule mwenye kuacha swalah. Katika maoni yake mengine hamkufurishi hata yule mwenye kuacha swalah. Kwa sababu mambo haya ni magumu na ya khatari. Pande zote mbili dalili zao ni zenye nguvu. Kwa ajili hiyo mtu anaweza kutumbukia katika kitu katika kujigonga, maono tofauti na mengineyo.

Kwa mtazamo wa ash-Shaafi´iy, Maalik na Abu Haniyfah wanaonelea kuwa mtu huyu sio kafiri. Lakini hata hivyo wote wameafikiana ya kwamba iwapo ataacha kwa kukanusha ni kafiri. Kuna maafikiano juu ya kwamba akiacha kwa kukanusha ni kafiri. Ama lau ataacha kwa sababu ya uvivu na uzembe, mmesikia namna ambavyo kuna baadhi ambao wanamkufurisha.

ash-Shaafi´iy, Maalik na maimamu wengine wengi, akiwemo Ahmad katika moja ya maoni yake, wanaonelea kuwa hakufuru isipokuwa tu pale ambapo atakanusha uwajibu wake. Kama tulivyosema kuna maoni tofauti juu ya yule asiyeswali lakini anakubali uwajibu wa swalah. Kuna ambao wanaonelea kuwa anatakiwa kuuawa. Kwa mfano akiacha swalah ya Dhuhr anatakiwa kuambiwa kutubia. Anatakiwa kuamrishwa kuswali Dhuhr kabla ya ´Aswr kuingia. Akikataa, auawe hali ya kuwa ni mtenda dhambi. Wale wanaomkufurisha wanaonelea kuwa auawe hali ya kuwa ni mwenye kuritadi kwa sababu ni kafiri. Wengine kama tulivyosema wanaona kuwa anauawa hali ya kuwa ni mtenda dhambi. Abu Haniyfah na maimamu wengine wanaonelea kuwa hatakiwi kuuawa. Badala yake wanaonelea kuwa anatakiwa kutiwa jela, kuaziriwa na kuadhibiwa mpaka pale ambapo ima ataanza kuswali au afe kabisa.

[1] 09:11

[2] 09:05

[3] at-Tirmidhiy (2621), an-Nasaa’iy (463) na Ibn Maajah (1079). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[4] at-Tirmidhiy (2619), an-Nasaa’iy (464) na Ibn Maajah (1078). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 407-408
  • Imechapishwa: 01/10/2017