38. Allaah hana yeyote anayeshirikiana wala kufanana Naye

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

36- Ametakasika kutokamana na wapinzani na washirika.

MAELEZO

Ametukuka kwa dhati Yake, uwezo Wake na ufalme Wake kutokamana na wapinzani na washirika. Washirika ni wale wenye kulingana na wenye kufanana. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hana yote hayo. Hakuna yeyote anayeshirikiana na Allaah, kushabihiana Naye wala kuwa sawa Naye. Haya ni kutokana na utukufu wa uwezo Wake na ufalme Wake. Sambamba na hilo Yeye yuko juu kwa dhati Yake, bi maana juu ya viumbe Wake wote.

Wala Allaah hana wakinzani. Hakuna kiumbe yeyote awezaye kukinzana Naye. Hakika Yeye anapolitaka jambo basi hakuna yeyote awezaye kuyazuia maamrisho Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Anapotaka kutoa hakuna yeyote awezaye kuzuia kile anachotaka kukitoa, Anapotaka kukizuia kitu hakuna yeyote awezaye kukitoa hicho alichokizuia:

اللَّهُمَّ لاَ مَانِعَ لما أَعْطَيْتَ وَلاَ مُعْطِي لِمَا مَنَعْتَ وَلاَ يَنْفَعُ ذَا الْجَدِّ مِنْكَ الجَدُّ

”Ee Allaah! Hakuna awezae kukizuia Ulichokitoa na wala kutoa ulichokizuia. Tajiri hanufaiki na utajiri wake mbele Yako.”[1]

Amesema (Ta´ala):

مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Rehema yoyote anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna wa kuizuia, na anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake – Naye ni Mwenye nguvu zisizoshindikana, Mwenye hekima.”[2]

Hana mshirika yeyote. Hana mpinzani yeyote pindi anapoamrisha au anapokataza jambo. Hilo ni tofauti na viumbe. Viumbe wako na wapinzani na wanavutana wao kwa wao. Viumbe wote wana wakinzani. Viumbe ni wenye kufanana inapokuja katika elimu, majina, miili, sifa, matendo na vile anavyomiliki, lakini hakuna yeyote anayefanana na kushirikiana na Allaah (Subhaanah).

[1] al-Bukhaariy (844) na Muslim (593).

[2] 35:02

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 54-55
  • Imechapishwa: 26/09/2019