37. Shubuha ya kwanza ya watu wa Tawassul na majibu juu yake

Watu hawa wana shubuha wanazozitumia kama hoja, kwa madai yao, wakidhani kuwa ndio dalili.

1- Shubuha ya kwanza: Wanasema huku ni kufanya ukatikati. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَابْتَغُوا إِلَيْهِ الْوَسِيلَةَ وَجَاهِدُوا فِي سَبِيلِهِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

”Enyi mlioamini!  Mcheni Allaah na tafuteni Kwake kujikurubisha. Fanyenyi Jihaad katika njia Yake mpate kufaulu.” (al-Maaidah 05:35)

Wakafasiri neno ukaribu/ukatikati (الْوَسِيلَةَ) ya kwamba ni kuweka baina yako wewe na Allaah mkatikati katika viumbe. Wamefasiri ukatikati namna hii. Vilevile katika maneno Yake (Ta´ala):

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ

Hao wanaowaomba [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia [na] kumkurubia kadri wanavyoweza na wanataraji rehema Zake.” (al-Israa´ 17:57)

Wakafasiri ukatikati katika Aayah hizi mbili kwamba makusudio ni kuweka mkatikati baina yao na baina ya Allaah. Tafsiri hii ni batili. Haikusemwa na yeyote katika maimamu wa tafsiri. Bali wamefasiri ukatikati kwamba ni utiifu na kujikurubisha Kwake kwa kumuabudu. Ukatikati ni njia inayofikisha kwa Allaah. Nayo ni kwa kumuabudu Mmoja pekee asiyekuwa na mshirika. Ukatikati ni ´ibaadah na utiifu na kufanya yale aliyoamrisha na kujiepusha na yale aliyokataza. Kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ

“Hao wanaowaomba [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia [na] kumkurubia kadri wanavyoweza na wanataraji rehema Zake na wanakhofu adhabu Yake.”

Maana ni kwamba wale wanaowaabudu Malaika na wanamuabudu al-Masiyh (´alayhis-Salaam) katika manaswara, Allaah amewaraddi kuwa wale ambao nyinyi mnawaabudu ni miongoni mwa waja Wangu, wanajikurubisha Kwangu na kuniabudu Mimi. Wao wenyewe hawamiliki chochote katika uola. Wao ni waja wanaojikurubisha kwa Allaah kwa kumuabudu, wanataraji rehema za Allaah na wanakhofu adhabu Yake. Kwa hiyo haijuzu kuwafanya wakatikati na njia ambapo mtu akawa anajikurubisha kwa Allaah kwa ukatikati wao. Amesema (Ta´ala):

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ

“Hao wanaowaomba… “

Wanawaomba washirikina katika Malaika na baadhi ya Mitume, kama al-Masiyh (´alayhis-Salaam), ni waja wa Allaah na hawana lolote katika dini hii.

يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ

“… [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia… “

Wao ni mafukara kwa Allaah na wanahitajia kutoka kwa Allaah.

وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ

“… na wanataraji rehema Zake na wanakhofu adhabu Yake.”

Vipi basi watafanywa kuwa waungu wanaoabudiwa pamoja na Allaah ilihali ni waja, wanakhofu adhabu ya Allaah, wanataraji rehema za Allaah na wanajikurubisha kwa Allaah? Hii ndio tafsiri ya Allaah ilivyofasiriwa na maimamu wa tafsiri za Qur-aan.

Imesemekana vilevile kwamba kuna watu waliokuwa wakiabudu baadhi ya majini. Majini yale yakasilimu. Wale waliokuwa wakiwaabudu hawakujua kuwa majini yale yamesilimu. Allaah akaeleza ya kwamba hawa mnaowaabudu badala ya Allaah wamesilimu na wamekuwa waja wa Allaah wanaojikurubisha kwa Allaah na kutaraji rehema Zake na wanaogopa adhabu Yake. Vipi watafanywa kuwa washirika pamoja na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pamoja na kuwa wao ni waja Wake, wanamuabudu Allaah, wanataraji rehema Zake na kuogopa adhabu Yake?

Aayah hii ina tafsiri mbili sahihi:

Ya kwanza: Ni wale wanaowaabudu Malaika na baadhi ya Mitume.

Ya pili: Kuna majini yalisilimu na wala hawakujua ya kwamba wanaowaabudu wamesilimu. Allaah akaeleza kuhusu wao.

Kwa hali yoyote maadamu hali ni hivyo, wao ni waja na wanajikurubisha kwa Allaah, wanataraji kupata rehema Yake na wanaogopa adhabu Yake. Kwa hiyo haijuzu kufanywa kuwa washirika pamoja na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hivyo tafsiri yao kwamba ukaribu/ukatikati (Wasiylah) kusema kwamba ni kuweka mkatikati katika viumbe baina yao na Allaah itakuwa imebatilika. Vilevile hoja yao itakuwa imeanguka – na himdi zote anastahiki Allaah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 09/08/2018