37. Radd kwa baadhi ya shubuha zinazotumika juu ya kushuka kwa Allaah


Wakatazama namna ambavyo jua linaizunguka ardhi, wakasema Atashuka vipi ilihali usiku unatofautiana kwa kutofautiana kwa miji? Jua ndio lenye kuizuguka ardhi. Hivyo sehemu ya ulimwengu kunakuwa ni mchana na sehemu nyingine inakuwa ni usiku. Hivi kwetu inakuwa ni mchana na kwa wengine inakuwa ni usiku na kinyume chake. Tunawaraddi kwa kuwaambia:

Sisi hatuingilii hili kwa kuwa hili ni jambo la Allaah. Yule ambaye ameweka usiku na mchana na akafanya kuwa vinapishana ndiye huyo huyo Aliyetukhabarisha kuwa hushuka (Subhaanahu wa Ta´ala). Sisi tunathibitisha kushuka na wala hatuingilii namna. Hatuulizi ni vipi anashuka theluthi ya usiku ilihali usiku unatofautiana kwa kutofautiana kwa miji. Mtu anaweza kuuliza hivi ikiwa inahusiana na kushuka kwa viumbe. Kuhusu kushuka kwa Muumba Yeye hushuka namna anavyotaka (Subhaanahu wa Ta´ala).

Wakasema tena kwamba kuteremka kunapelekea kufanya harakati na kutoka sehemu kwenda nyingine. Wakauliza kama Allaah hutoka kwenye ´Arshi Yake na kuteremka kwenye mbingu ya dunia na kama anafanya harakati. Tunawaraddi kwa kuwaambia: huku ni kutafiti namna. Sisi tunasema kuwa Anashuka namna anavyotaka. Hatujui namna. Allaah hushuka namna anavyotaka. Hakika Yeye juu ya kila jambo ni muweza. Yeye ndiye ambaye ameumba mbingu na ardhi. Hivyo hatuingii ndani ya hili.

Sisi tunathibitisha kushuka, kama ilivyokuja, pindi kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku. Tunathibitisha hilo na wakati huo huo tunaliamini. Hatujali ubabaishaji wa watu hawa ambao wanataka kumkosoa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni kama kwamba wanamwambia: “Ee Mola wetu! Hakika kushuka hakulingani na Wewe kutokana an sababu hii na ile.” Wanamkosoa Allaah (Jalla wa ´Alaa) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni kama kwamba wao ni wajuzi zaidi kuliko Allaah na ni wajuzi zaidi kumtambua Allaah (Jalla wa ´Alaa) kuliko Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Huku ni kuwa na utovu wa adabu kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Allaah anathibitisha kuwa anashuka na wao wanakanusha na wanasema ikiwa anafanya hivo, basi itamlazimu hili na lile. Haya ni malazimisho batili.