37. Ni ipi hukumu ya mlinganizi kuita katika swalah za pamoja?

Swali 37: Kuna vijana wanaotaka kuwalingania watu katika dini ya Allaah na kuwalea vijana juu ya Uislamu. Wanatumia baadhi ya barnamiji kama swalah za pamoja katika baadhi ya siku. Ni ipi hukumu ya kitendo chao[1]?

Jibu: Da´wah inatakiwa iwe juu ya Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haikupokelewa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia Maswahabah wake (Radhiya Allaahu ´anhum):

“Tuache tufunge siku moja swawm ya Sunnah ya pamoja.”

Kitu kilichopokelewa tu ni kuwa Salamah bin al-Akwa´ (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha mwenye kusilimu akiri kati ya watu:

“Mwenye kufunga atimize swawm yake. Aliyekula asile kitu zaidi na badala yake atimize swawm yake.”[2]

Katika upokezi mwingine ar-Rubayy´ bin Mu´awwidh bin ´Afrah ameeleza:

“Asubuhi ya ´Aashuuraa´ Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituma mjumbe kwenda katika vijiji vya Aswaar nje ya al-Madiynah akisema: “Aliyeamka asubuhi hali ya kuwa amefunga basi atimize swawm yake. Aliyeamka asubuhi hali ya kuwa hakufunga basi atimize siku yake iliyobaki.”[3]

Mwanzoni mwa Uislamu, kabla ya Ramadhaan kuwa faradhi, ilikuwa ni wajibu kufunga ´Aashuuraa´. Anayetaka kuwafunza mabarobaro haifai akamkalifisha yeyote kufunga swawm ya pamoja. Ni Bid´ah ikiwa malengo ni kumuabudu Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuzua katika amri yetu hii yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”[4]

Badala yake mlinganizi anatakiwa kuwabainishia wanafunzi wake fadhila za swawm na fadhila zinazopatikana katika kufunga jumatatu na alhamisi, masiku meupe au siku tatu katika Ramadhaan. Asimwamrishe yeyote kufunga siku maalum. Awaache watu wafunge wao wenyewe kwa kutaka kwao. Akiwaamrisha kufunga basi amefanya lililopendekezwa kwenda katika faradhi. Ni uwekaji Shari´ah ambao haukuidhinishwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hukumu zinatakiwa ziwe kama zilivyo na kama zilivyokuwa pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokufa. Mlinganizi anatakiwa tu kubainisha na kutaja zile Hadiyth zinazovutia katika matendo mema bila ya kuwalazimisha kitu. Kama jinsi tunawajibika kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kizazi chake katika mambo yote, kadhalika tunawajibika kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi tunapoita katika dini ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

[1] Kutoka “Fath-ur-Rabb al-Waduud” (1/252).

[2] Ahmad (16508).

[3] Muslim (1919).

[4] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaas-Swiyaam, uk. 53-56
  • Imechapishwa: 12/06/2017