37. Kutoa Salaam


153- ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba kuna mtu alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Uislamu upi bora. Akajibu:

“Kulisha chakula na kumsalimia unayemjua na usiyemjua.”

154- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hamtoingia Peponi mpaka muamini na hamtoamini mpaka mpendane. Nisikuelezeni kitu ambacho mkikifanya kitawafanya kupendana? Enezeni Salaam baina yenu.”

155- ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema:

“Kuna sifa tatu. Mwenye kuwa nazo basi amekusanya imani; uadilifu juu ya nafsi yako, kuwatolea Salaam viumbe na kujitolea katika kipindi kizito.”

156- ´Imraan bin Husayn (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema:

“Kuna mtu alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema:

السَّلاَمُ عَلَيْكُمْ

“as-Salaam ´alaykum.”

Akamuitikia kisha mtu yule akakaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Kumi.” Kisha akaja mtu mwengine na kusema:

السَّلام عَلَيْكُمْ وَرحمة الله

“as-Salaam ´alaykum wa Rahmatullaah.”

Akamuitikia kisha mtu yule akakaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ishirini.” Kisha akaja mtu mwengine na kusema:

السَّلاَمُ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَةُ اللهِ وَبَرَكَاته

“as-Salaam ´alaykum wa Rahmatullaahi wa Barakaatuh.”

Akamuitikia kisha mtu yule akakaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Thalathini.”

157- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu walio na haki zaidi kwa Allaah ni wale wenye kuanza kwa Salaam.”

158- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Inatosheleza katika kundi linalopita mmoja wao akatoa Salaam na inatosheleza katika kundi linalokaa mmoja wao akaitikia Salaam.”

159- Anas (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita pembezoni mwa watoto wanaocheza akawatolea Salaam.”

160- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wakati mmoja wenu anapofika katika majlisi awatolee Salaam. Akitaka kukaa, akae. Akitaka kusimama na kwenda awatolee Salaam. [Salaam] ya kwanza haina haki zaidi kuliko ile ya pili.”

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 100-102
  • Imechapishwa: 21/03/2017