37. I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya Qur-aan na kwamba haikuumbwa

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika hayo kunaingia vile vile kuamini ya kwamba Yuko karibu na viumbe Vyake na ni Mwenye Kuwajibu, kama Alivyojumuisha baina ya hayo katika Kauli Yake:

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi niko karibu na Naitikia maombi ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi wapate kuongoka.” (02:186)

Na kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia Maswahabah waliponyanyua sauti zao kwa Dhikr:

“Enyi watu! Zihurumieni nafsi zenu! Kwani hakika hamumuombi ambaye ni kiziwi wala asiyekuwepo. Hakika Yule mnayemwomba ni Mwenye Kusikia Mwenye kuona na Aliye karibu. Hakika yule mnayemwomba Yuko karibu na mmoja wenu kuliko shingo ya mpando wenu.”

Na yaliyotajwa katika Kitabu na Sunnah kuhusu Ukaribu Wake na Kuwa Kwake pamoja, hayapingani na yaliyotajwa kuhusu kuwa Kwake juu ya viumbe, kwa kuwa Yeye (Subhaanah) hakuna kitu mfano Wake katika Sifa Zake zote. Naye Yuko juu kabisa kwa Ukaribu Wake na Yuko Karibu kwa Ukuu Wake.

Katika kumuamini Allaah na Vitabu Vyake kunaingia kuamini ya kuwa Qur-aan ni Maneno ya Allaah, imeteremshwa na haikuumbwa. Uteremsho wake umeanza kutoka Kwake na Kwake itarudi. Allaah Kaongea Kwayo Kauli ya kihakika. Qur-aan hii iliyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Maneno ya Allaah ya kihakika na sio maneno ya mwengine. Na wala haijuzu kusema ya kwamba ni hikaaya au ibara ya Maneno ya Allaah, bali wanapoisoma watu au kuiandika kwenye misahafu, kwa kufanya hivyo haijatoka kuwa Maneno ya Allaah ya kihakika. Kwani hakika Maneno yananasibishwa na yule aliyeyatamka mwanzo, na si kwa yule aliyeyawakilisha (kuyafikisha). Hivyo ni Maneno ya Allaah; herufi na maana yake. Maneno ya Allaah sio herufi bila ya maana na wala sio maana bila ya herufi.

MAELEZO

Katika hayo kunaingia vile vile kuamini ya kwamba Yuko karibu na viumbe Vyake… – Mwandishi (Rahimahu Allaah) amebainisha kuwa kunaingia katika kumuamini Allaah, majina na sifa Zake kuamini pia ya kwamba Yeye yukaribu na ni mwenye kuitikia (Subhaanahu wa Ta´ala). Yeye yuko juu ya ´Arshi. Hili halipingani na kuwa Kwake karibu na mwenye kuitikia (Subhaanahu wa Ta´ala). Yeye yuko juu kabisa kwa Ukaribu Wake na yuko Karibu kwa Ukuu Wake kama alivyosema mwandishi. Yeye yukaribu na ni mwenye kuitikia na wakati huo huo yuko juu (Subhaanahu wa Ta´ala). Yuko juu ya ´Arshi, juu ya mbingu zote na juu ya viumbe vyote. Kwa jili hii amesema (Ta´ala):

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi niko karibu na Naitikia maombi ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi wapate kuongoka.”(02:186)

Hakika (Subhaanah) yuko karibu kwa mwenye kumuomba na ni Mwenye kuwaitikia waja Wake hekima Yake ikionelea kufanya hivyo. Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika yule mnayemwomba Yuko karibu na mmoja wenu kuliko shingo ya mpando wenu.”

ilikuwa pale alipowasikia baadhi ya Maswahabah zake wananyanyua sauti zao safarini ndipo akawaambia:

“Hakika hamumuombi ambaye ni kiziwi wala asiyekuwepo. Hakika Yule mnayemwomba ni Mwenye Kusikia Mwenye kuona na Aliye karibu. Hakika yule mnayemwomba Yuko karibu na mmoja wenu kuliko shingo ya mpando wenu.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Hakika Yule mnayemwomba ni Mwenye Kusikia, Mwenye kuona na Yuko karibu. Hakika Yuko karibu na mmoja wenu kuliko shingo ya mpando wenu.”

Pamoja na kuwa (Subhaabah) yuko juu ya ´Arshi halipingani kitu na kuwa Kwake karibu, Mwenye kutikia na anasikia du´aa ya mwenye kumuomba. Yeye ndiye Mwenye kusikia du´aa, yuko karibu kwa kuitikia ni Mwenye kusikia na kuitikia (Subhaanahu wa Ta´ala). Amekariri hilo katika Aayah nyingi ambapo amejisifu ya kwamba ni Mwenye kusikia, anazisikia siri na minong´onezo na hakuna kinachojifichika Kwake (Jalla wa ´Alaa). Vivyo hivyo katika Hadiyth. Yaliyotajwa kuhusu kuwepo Kwake juu hakupingani kitu na kuwepo Kwake karibu na pamoja na viumbe. Yeye yuko pamoja na waja Wake kwa ujuzi Wake na kuwaona:

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ

“Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.” (57:04)

Vilevile yuko pamoja na mawalii Wake kwa ujuzi Wake, kuwahifadhi, kuwanusuru na kuwapa nguvu (Subhaanahu wa Ta´ala).

Ni wajibu kwa kila muumini mwanaume na mwanamke kuamini hilo na kwamba Yeye ni Mwenye kusikia na yuko karibu. Uwepo Wake (Jalla wa ´Alaa) juu ya ´Arshi haupingani kitu na kuwakaribia Kwake waja Wake na kuzisikia Kwake du´aa zao (Jalla wa ´Alaa). Yeye ni Mwenye kusikia na yukaribu na wakati huo huo yuko juu na ni Mkuu (Jalla wa ´Alaa). Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

”Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Na Yeye ndiye Aliye juu, na ndiye Mkuu.” (02:255)

إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ

Kwake Pekee linapanda neno zuri na amali njema Hukipa hadhi.” (35:10)

Katika kumuamini Allaah na Vitabu Vyake kunaingia kuamini ya kuwa Qur-aan… – Katika kumuamini Allaah ni pamoja vilevile na kuamini kuwa Qur-aan ni Maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Katika kuamini Vitabu vya Allaah ni pamoja na kuamini vilevile kwamba Qur-aan ni Kitabu kilichoteremshwa kwa mja na Mtume Wake ambaye ndiye Nabii wa mwisho, Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Qur-aan ni maneno ya Allaah, sawa herufi na maana yake. Ni wajibu kuamini kuwa ni maneno ya Allaah na imeteremshwa haikuumbwa. Imeanza kutoka Kwake na Kwake itarudi. Pale inapoandikwa kwenye misahafu, inaposomwa na inapohifadhiwa haipingani na kuwa ni maneno ya Allaah. Imehifadhiwa kwenye vifua, imeandikwa kwenye misahafu na inasikiwa na masikio. Pamoja na haya yote bado ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall), sawa herufi na maana yake.

Na wala haijuzu kusema ya kwamba ni hikaaya au ibara ya Maneno ya Allaah… – Haijuzu kusema kuwa Qur-aan ni hikaaya au ni ibara ya maneno ya Allaah kama wanavyosema Ashaa´irah na Kullaabiyyah na wengineo. Qur-aan ni maneno ya Allaah herufi na maana yake na sio ibara wala hikaaya ya maneno ya Allaah. Ni maneno ya Allaah kwa dhati yake. Maneno Yake (Ta´ala):

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ

”Allaah, hakuna mungu wa haki ila Yeye – Aliyehai daima, Msimamizi wa kila kitu.” (02:255)

ni maneno ya Allaah.

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Sifa njema na shukurani zote ni za Allaah, Mola wa walimwengu.” (01:01)

ni maneno ya Allaah.

وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا

”Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo.” (02:255)

ni maneno ya Allaah.

Maneno ya Allaah sio herufi bila ya maana… – Kila Aayah na kila neno yote hayo ni maneno ya Allaah, kuanzia mwanzo wake mpaka mwisho wake, sawa herufi na maana yake. Maneno ya Allaah sio harefi pasi na maana na wala sio maana pasi na herufi.

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ

”Allaah, hakuna mungu wa haki ila Yeye – Aliyehai daima, Msimamizi wa kila kitu.” (02:255)

Haya ni maneno ya Allaah.

Kadhalika maana yake kuhusiana na uhai, kuyasimamia Kwake mambo, kuyalinda na kuyahifadhi Kwake mambo yote haya ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

قُلْ مَن يَكْلَؤُكُم بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ مِنَ الرَّحْمَـٰنِ

“Sema: “Nani [awezaye] kukulindeni usiku na mchana kutokana na [adhabu ya] Mwingi wa Rahmah?”” (21:42)

إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ

“Kwake Yeye linapanda neno zuri na kitendo chema hukinyanyua.” (35:10)

فَالْحُكْمُ لِلَّـهِ الْعَلِيِّ الْكَبِيرِ

“Basi [leo] hukumu ni ya Allaah Pekee, Aliye juu, Mkubwa kabisa.” (40:12)

إِنَّهُ سَمِيعٌ قَرِيبٌ

“Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Yu karibu.” (34:50)

إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Hakika Allaah ni Mwenye kusikia, Mjuzi.” (02:181)

وَأَنَّ اللَّـهَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Allaah ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.” (24:20)

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwa yote haya, sawa herufi na maana yake, ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com