37. Imani ni maneno na vitendo, inazidi na inashuka

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Imani ni maneno na matendo, inapanda na kushuka. Kama ilivyokuja katika mapokezi:

“Waumini walio na imani kamilifu zaidi ni wale walio na tabia bora zaidi.””[1]

MAELEZO

Imani ni maneno na vitendo; maneno ya moyo na ya ulimi pamoja na matendo ya moyo na ya viungo vya mwili. Tunaweza pia kusema kuwa imani ni maneno, vitendo na kuamini na kwamba inazidi kwa matendo mema na inashuka kwa maasi. Hii ndio tafsiri ya imani kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Vilevile Khawaarij wanaamini kuwa imani ni maneno, vitendo na kuamini. Lakini hata hivyo wanaonelea kuwa imani haizidi na wala haipungui. Pale ambapo muislamu anapofanya dhambi kubwa basi mara moja anatoka katika Uislamu, ndivyo wanavyosema.

Wanakabiliwa na Murji-ah wanaosema kuwa imani kule kusadikisha kwa moyo peke yake, au kule kutambua kwa moyo, kama wanavyosema Jahmiyyah. Murji-ah waliopindukia wanaonelea kuwa imani ni kule kusadikisha kwa moyo peke yake.

Murji-ah al-Fuqahaa´ wanaonelea kuwa imani ni kuamini kwa moyo na maneno ya ulimi. Hawaingizi matendo katika imani.

Ahl-us-Sunnah wanaonelea kuwa imani ni matendo ya moyo na matendo ya viungo vya mwili baada ya kusadikisha. Imani imekusanya kule kuamini na matendo ya moyo kukiwemo kumuogopa Allaah, kumpenda, kumtarajia, kuwa na shauku Kwake na kumtegemea. Yote haya ni katika vitendo vya moyo. Ni katika kilele cha imani. Imani haiwezi kupatikana isipokuwa kwa mambo hayo. Kadhalika matendo ya viungo vya mwili kama vile swawm, swalah, zakaah, jihaad na mambo mengine ya wajibu. Hata kuondosha kitu chenye kudhuru kwenye barabara ni katika imani:

“Imani imegawanyika zaidi ya sehemu sabini. Ya  juu yake ni neno “Hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah” na ya chini yake ni kuondosha kitu chenye kudhuru katika  njia. Hayaa ni sehemu katika imani.”[2]

Imani hii inazidi kwa matendo mema na inapungua kwa maasi. Inapanda mpaka inakuwa kama mlima na inashuka mpaka inakuwa na uzito chini kuliko mdudu chungu.

Murji-ah wao wanaonelea kuwa imani haizidi na wala haipungui. Kwa sababu wanaonelea kuwa imani ni kule kusadikisha peke yake na ndio maana haipungui. Wanadai kuwa ule usadikishaji wake ukiingiwa na upunguaji basi hawi tena muumini. Kwa hivyo haipungui. Wanaonelea kuwa imani si yenye kutofautiana kati ya watu. Wanaonelea kuwa watu wote wana imani ya sawa. Kwa mujibu wao mtu muovu kabisa wa watu imani yake ni sawa ya Mitume, wakweli na Malaika. Huu ni upotevu mkubwa. Khawaarij ndio wanaokabiliana nao katika upotevu wao.

Murji-ah waliopindukia ndio waovu zaidi kwa kuwa wanaibomoa Shari´ah kwa ´Aqiydah hii mbovu kabisa. Khawaarij ni wabaya pia kwa sababu wanawakafirisha Ummah, wanawaua waislamu na wanahalalisha damu na mali zao. Pale ambapo mtu anapofanya dhambi kubwa tu, kama uzinzi, uibaji na mauaji, wanaonelea kuwa ni kafiri. Huu ni uongo, upotevu na ufahamu mbaya. Ni kwa nini Allaah ameamrisha mwizi aadhibiwe?

وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا جَزَاءً بِمَا كَسَبَا نَكَالًا مِّنَ اللَّـهِ ۗوَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Mwizi mwanamume na mwizi mwanamke wakateni mikono yao – ni malipo kwa yale waliyoyachuma; [Shari´ah hii] ni makemeo makali kutoka kwa Allaah. Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[3]

Ni kwa nini Allaah ameamrisha walevi kuadhibiwa? Pindi mtu mmoja aliyekunywa pombe alipoletwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo mtu mmoja akamlaani, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Usimlaani. Kwani hakika anampenda Allaah na Mtume wake.”[4]

Ni vipi muumini ataadhibiwa na kukufurishwa wakati mmoja? Adhabu inamsafisha. Vivyo hivyo yule mtu anayezini kisha akaadhibiwa anasifika kwa dhambi yake. Kuhusu kafiri, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kubadilisha dini yake muueni.”[5]

Madhambi kama vile uzinzi, mauaji na kunywa pombe ni madhambi makubwa na mazito kabisa katika Uislamu, lakini hayamtoi mtu katika Uislamu. Badala yake anatakiwa kutekelezewa adhabu hapa duniani na Aakhirah vilevile ikiwa Allaah hatomsamehe. Lakini hata hivyo hatoki katika Uislamu. Hapana shaka ya kwamba dhambi ya mpwekeshaji huu itamtoa Motoni na kumwingiza Peponi.

[1] Abu Daawuud (4682) na at-Tirmidhiy (1162). Nzuri na Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[2] Muslim (35).

[3] 05:38

[4] al-Bukhaariy (6780).

[5] al-Bukhaariy (3017).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 405-407
  • Imechapishwa: 25/09/2017