Swali 36: Mtu akija msikitini siku ya ijumaa akakutana swalah imekwishaswaliwa ambapo akampata mtu ambaye amebakiwa na Rak´ah moja – je, akamilishe Rak´ah hii kama Dhuhr au ijumaa? Akijiunga naye mtu mwengine baada ya kuswali Rak´ah moja – je, naye aikamilishe kama Dhuhr au kama ijumaa[1]?

Jibu: Kinachomlazimu aikamilishe kama Dhuhr kwa sababu ijumaa imekwishapita. Swalah ya ijumaa inadirikiwa kwa Rak´ah moja akiwahi Rak´ah ya pili pamoja na imamu. Katika hali hiyo ataiswali kama swalah ya ijumaa.

Ama akija baada ya salamu au akaja baada ya Rak´ah ya pili katika Tashahhud au katika hali ya Sujuud katika Rak´ah ya pili, basi hatoiswali kama ijumaa. Lakini ataiswali kama Dhuhr. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayewahi Rak´ah moja ya ijumaa, basi aongezee juu yake nyingine na hivyo swalah yake imetimia.”[2]

Kinachopata kufahamika ni kwamba akiwahi chini ya Rak´ah moja, basi hazingatiwi kuiwahi ijumaa. Lakini ataiswali kama Dhuhr. Hili ndilo lililowekwa katika Shari´ah.

Akijiunga na mtu ambaye anakidhi akaswali naye basi aswali pamoja naye Dhuhr na asiswali ijumaa.

Kidokezo kingine ni kwamba hayo yafanyike baada ya kupondoka kwa jua. Ama ikiwa ijumaa imeswaliwa kabla ya jua kupondoka, basi asiswali Dhuhr isipokuwa baada ya jua kupondoka. Kwa sababu inafaa kuswali swalah ya ijumaa kabla ya jua kupondoka mida ya saa sita kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanazuoni. Lakini bora na salama zaidi iswaliwe baada ya jua kupondoka, kama yalivyo maoni ya wanazuoni wengi. Kuhusu Dhuhr haifai ikaswaliwa isipokuwa baada ya jua kupondoka kwa maafikiano ya waislamu.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/329-330).

[2] at-Tirmidhiy (482), an-Nasaa´iy (554) na Ibn Maajah (1114).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 75
  • Imechapishwa: 03/12/2021