Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

36- Anamwongoza amtakaye. Analinda na kuafu kutokana na fadhilah. Anapotosha, anakosesha nusura na kujaribu kwa uadilifu.

MAELEZO

Allaah (Subhaanah) anamwongoza na anampoteza amtakaye. Yote haya ni kutokana na mipango na makadirio ya Allaah. Lakini anamwongoza yule anayejua kuwa anastahiki kuongozwa, anaipupia na kuikubali. Katika hali hiyo Allaah anamfanyia wepesi wa uongofu. Upande wa pili anampoteza yule ambaye anapuuzilia mbali uongofu na kheri. Huyu Allaah anampoteza ikiwa ni adhabu kwake juu ya kupuuza kwake na kutotaka kwake kheri. Ameliweka hilo wazi katika maneno Yake (Ta´ala):

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ

“Basi yule anayetoa [mali zake] na akamcha Allaah na akasadikisha al-Husnaa, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo mepesi.”[1]

Sababu ikawa ni yenye kutoka kwa mja na makadirio ni kutoka kwa Allaah:

وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ  فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ

“Ama yule afanyaye ubakhili na akajiona amejitosheleza na akakadhibisha al-Husnaa, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo magumu.”[2]

Hapa pia sababu ikawa ni yenye kutoka kwa mja na makadirio ni kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) kama adhabu kwake. Kwa msemo mwingine Allaah anamkadiria mtu kuongoka kwa ajili ya kumtukuza na kumuheshimisha kutokana na kupenda kwake kheri na uongofu. Hivyo anamsahilishia kuweza kuutendea kazi. Sambamba na hilo mja huyo ndiye ananufaika na si kwamba Allaah (´Azza wa Jall) ndiye ananufaika.

Kuhusu kuwapoteza wapotofu, Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anafanya hivo kutokana na uadilifu wake. Allaah anawaadhibu kwa sababu ya kupuuza kwao haki na kutomtii Allaah (´Azza wa Jall). Allaah hakuwadhulumu chochote. Tunaona kuwa Allaah anasema:

وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

“Allaah hawaongoi watu madhalimu.”[3]

وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ

“Allaah hawaongoi watu mafasiki.”[4]

Amefanya dhuluma, kufuru na ufasiki kuwa ni kikwazo cha uongofu. Hivi ndivo Allaah anawalipa waja kutokana na matendo yao; ni uadilifu na sio dhuluma:

كَذَٰلِكَ فَعَلَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّـهُ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ

“Hivyo ndivyo walivyofanya wale wa kabla yao. Allaah hakuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao wenyewe.”[5]

Haimstahikii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kuwatukuza watu wa sampuli hii. Kadhalika haimstahikii Yeye kuyapoteza na kuyapuuza matendo mema ya watendaji:

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ وَخَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَلِتُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ

“Je, wanadhania wale waliochuma mabaya Tuwafanye wawe sawa na wale walioamini na wakatenda mema na pia sawasawa uhai wao na kufa kwao? – uovu ulioje wanaouhukumu! Allaah ameumba mbingu na ardhi kwa haki na ili ilipwe kila nafsi kwa yale iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa.”[6]

أَفَنَجْعَلُ الْمُسْلِمِينَ كَالْمُجْرِمِينَ مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ

”Je, Tuwafanye waislamu sawa kama wahalifu? Mna nini nyinyi! Vipi mnahukumu?”[7]

Allaah anajitakasa kutokamana na dhuluma kama hii:

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

“Je, Tuwajaalie wale walioamini na wakatenda mema kama wenye kueneza ufisadi ardhini au tuwajaalie wachaji kama waovu?”[8]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hayapotezi matendo mema ya wenye kutenda kama ambavo hamuadhibu yeyote kwa jambo ambalo hakufanya:

مَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“Hamlipwi isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda.”[9]

[1] 92:05-07

[2] 92:08-10

[3] 02:258

[4] 05:108

[5] 16:33

[6] 45:21-22

[7] 68:35-36

[8] 38:28

[9] 37:39

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 52-54
  • Imechapishwa: 26/09/2019