36. Radd kwa wanaokanusha Allaah kushuka kwenye mbingu ya dunia


Kwa vile Hadiyth hii imepokelewa kwa mapokezi mengi (Mutawaatir) na wakaona hawana namna ya kuikwepa, sasa wakataka kujibebetua ili wajikwamue nayo. Wakasema:

“Hushuka”

maana yake ni amri Yake ndio hushuka. Tunawaraddi kwa kuwaambia: katika Hadiyth imekuja ya kwamba Husema: “Ni nani anayeniomba msamaha nimsamehe? Ni nani anayeniomba nimpe? Kuna mwenye kutubia nimsamehe? Kuna mwenye kuniomba msamaha nimghufurie? Kuna kwenye kuniomba nimpe?”[1]

Je, amri inaweza kusema:

“Ni nani anayeniomba nimpe? Ni nani anayeniomba msamaha nimsamehe?”

Hili ni batili. Mwenye kusema haya ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Wakasema:

“Hushuka Mola wetu.”

maana yake ni Malaika miongoni mwa Malaika ndiye mwenye kushuka. Tunawaraddi kwa kuwaambia: Je, Malaika ndiye mwenye kusema:

“Ni nani mwenye kuniomba msamaha? Ni nani mwenye kuniomba? Ni nani mwenye kutubia nimsamehe?”

Hivi kweli Malaika anaweza kusema haya au yanasemwa na Mola (Subhaanahu wa Ta´ala)? Bila shaka ni Mola (Jalla wa ´Alaa).

Kwa hivyo makusudio sio kwamba amri wala Malaika ndiye mwenye kushuka. Kwa kuwa si amri wala Malaika vyote viwili hakuna mwenye kuweza kutamka maneno haya yaliyokuja katika Hadiyth.

[1] al-Bukhaariy (1145) na Muslim (168) na (758)