36. Misimamo mbalimbali ya watu juu ya Aayah na Hadiyth za sifa

Makusudio ya watu ni wale wanaojinasibisha na Uislamu. Waislamu wamegawanyika katika makundi sita inapokuja katika zile Aayah na Hadiyth zinazozungumzia juu ya sifa:

1- Makundi mawili yanaona kuwa zinatakiwa kupitishwa kama zilivyo.

2- Makundi mawili yanaona kuwa hazitakiwi kupitishwa kama zilivyo.

3- Makundi mawili yamenyamaza.

Wale wenye kuonelea kuwa zinatakiwa kupitishwa kama zilivyo ni makundi mawili:

1- Mushabbihah. Ni wale ambao wanaonelea kuwa sifa za Allaah ni kama sifa za viumbe. ´Aqiydah yao ni batili na imekaripiwa na Salaf.

2- Salaf ambao wameonelea kuwa zinatakiwa kupitishwa kama zilivyo kwa njia inayolingana na Allaah (´Azza wa Jall). ´Aqiydah yao ndio sahihi kabisa. Dalili yake iko katika Qur-aan, Sunnah na akili timamu waziwazi. Dalili ima ni ya uhakika kabisa au ni ya dhana ilio na nguvu.

Tofauti kati ya makundi haya mawili, hilo la kwanza linamfananisha Allaah na viumbe wakati hili la pili linakemea ´Aqiydah hii.

Endapo Mushabbihah watasema kuwa wao hawaelewi jengine juu ya elimu, kushuka na mkono wa Allaah isipokuwa kama wanavyoelewa elimu, kushuka na mkono wa kiumbe, wataraddiwa kwa njia zifuatazo:

1- Akili na dalili za Kishari´ah vyote viwili vimejulisha utofauti kati ya Muumba na kiumbe katika sifa Zake zote. Sifa za Muumba zinalingana na Yeye na sifa za kiumbe zinalingana na yeye. Moja katika dalili za Kishari´ah yenye kuonyesha utofauti kati ya Muumba na kiumbe ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

أَفَمَن يَخْلُقُ كَمَن لاَّ يَخْلُقُ أَفَلا تَذَكَّرُونَ

“Hivi yule Anayeumba utamlinganisha na ambaye haumbi? Mbona hamfikirii?”[2]

Ama mtazamo wa kiakili, tunauliza ni vipi Muumba mkamilifu, ambaye ni mkamilifu kwa njia zote na ambaye ukamilifu ndio umelazimiana na dhati Yake, anaweza kufanana na kiumbe ambaye ni mpungufu na ambaye mapungufu ndio yamelazimiana na dhati yake na ambaye ni muhitaji wa ambaye ataikamilisha?

2- Je, mnajua kuwa dhati ya Allaah haifanani na dhati ya kiumbe? Wataitikia ndio. Basi ni lazima mwelewe kuwa sifa za Allaah hazifanani na sifa za viumbe kwa sababu kuzungumzia juu ya sifa ni kama kuzungumzia juu ya dhati. Mwenye kutofautisha kati ya hivyo basi amejigonga.

3- Sisi tunaona namna ambavyo viumbe wana sifa zilizo na majina yenye kufanana lakini namna tofauti. Kwa mfano mkono wa mwanaadamu sio kama mkono wa mnyama. Ikiwa inawezekana viumbe wakawa na sifa zilizo na jina moja na namna tofauti, basi utofauti kati ya Muumba na kiumbe ni mkubwa zaidi. Utofauti kati ya hao wawili ni jambo la wajibu.

[1] 42:11

[2] 16:17

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 86-87
  • Imechapishwa: 13/05/2020