36. Mambo yenye kufanya imani ikazidi


Imani inazidi kwa sababu mbali mbali:

1- Kujua majina na sifa za Allaah. Kadri ambavyo mtu atazidi kuyatambua na kujua maana na athari yake, ndivyo jinsi imani na mapenzi na kumuadhimisha Mola kutakavyozidi.

2- Kuzitafakari ishara za Allaah za kilimwengu na Aayah za Kishari´ah. Kadri ambavyo mtu atazidi kuzitafakari na kuzingatia ile nguvu kubwa na hekima kubwa inayopatikana ndani yake, ndivyo jinsi imani na yakini yake itakavyozidi.

3- Kutenda matendo mema kwa kujikurubisha kwa Allaah (Ta´ala). Imani inazidi kutegemea na ule uzuri, sampuli na wingi wa matendo. Kadri ambavyo kitendo kitakuwa kizuri zaidi, ndivyo jinsi imani itavyozidi. Uzuri wa kitendo unatokamana na Ikhlaasw na kule kuafikiana na Shari´ah.

Kuhusu sampuli ya kitendo, hakika cha wajibu ni bora zaidi kuliko kilichopendekezwa. Baadhi ya vitendo vimekokotezwa na ni bora zaidi kuliko vingine. Kadri jinsi kitendo kitakuwa bora zaidi, ndivyo jinsi imani inavyozidi.

Kuhusiana na wingi wa matendo, imani inazidi kadri jinsi matendo ni mengi. Kwa sababu matendo yanaingia katika imani, si ajabu ikazidi pale ambapo mtu anazidisha matendo.

4- Kuacha maasi kwa ajili ya kumuogopa Allaah (´Azaa wa Jall). Kila ambavyo mtu ana hima ya kufanya maasi fulani, ndivyo jinsi imani ya mtu inazidi kuwa na nguvu zaidi kwa kuyaacha. Mtu kuyaacha ilihali ana hima ya hali ya juu, ni dalili yenye kuonesha kuwa imani yake ina nguvu kabisa na kuwa anatanguliza yale anayoyapenda Allaah na Mtume Wake mbele ya matamanio yake.

Imani inapungua kwa sababu mbali mbali:

1- Mtu kuwa mjinga wa kutomjua Allaah (Ta´ala) na majina na sifa Zake.

2- Mtu kughafilika na alama za Allaah za kilimwengu na za kidini na hukumu na kuyapa mgongo. Yanasababisha moyo kuwa na maradhi au kufa kabisa kwa vile matamanio na utata vimeshika nafasi juu yake.

3- Kufanya maasi. Imani inashuka kwa kutegemea na sampuli ya maasi, kiwango chake na kuyachukulia usahali.

Kuhusiana na sampuli na viwango vyake, imani inashuka kwa madhambi makubwa kuliko inavyoshuka kwa madhambi madogo. Imani inashuka zaidi kwa kuua nafsi isiyokuwa na hatia kuliko mtu anapochukua mali ya mtu pasi na haki. Imani inashuka zaidi kwa dhambi mbili kuliko inavyoshuka kwa kufanya dhambi moja na kadhalika.

Ama kuhusu kuchukulia usahali maasi, imani inashuka zaidi ikiwa inatokamana na mtu ambaye khofu yake kwa Allaah ni dhaifu kuliko inavyoshuka pindi inatokamana na mtu ambaye anamuadhimisha zaidi Allaah na ni mwenye kumuogopa zaidi.

Kuhusu kupupia maasi, imani inashuka zaidi ikiwa yanafanywa na mtu ambaye upupiaji wake wa maasi una udhaifu kuliko yanapofanywa na mtu ambaye upupiaji wake wa maasi una nguvu zaidi. Ndio maana ikawa jeuri ya fakiri na uzinifu wa mtumzima ni jambo lina dhambi kubwa kuliko jeuri ya mtu ambaye ni tajiri na uzinifu wa kijana. Hadiyth inasema:

“Watu aina tatu Allaah hatowasemeza, hatowatazama siku ya Qiyaamah na wala Hatowatakasa na watakuwa na adhabu kali.”[1]

Kati yao ametaja mzee ambaye ni mzinifu na fakiri mwenye jeuri kutokamana na udhaifu wao katika kupupia dhambi hizi.

4- Kuacha utiifu. Imani inashuka kwa kuacha utiifu. Inashuka kwa kutegemea na uzito wa utiifu huo. Kadri ambavyo utiifu utakuwa umesisitizwa zaidi, ndivyo jinsi imani inashuka zaidi kwa kuacha kuufanya. Imani inaweza kutoweka kabisa kabisa kwa mfano mtu anaacha kuswali.

Kushuka kwa imani kwa kuacha utiifu kumegawanyika aina mbili:

Kwanza: Aina ambayo mtu anaadhibiwa kwayo na ni kule mtu kuacha kitu cha wajibu pasi na udhuru.

Pili: Aina ambayo mtu haadhibiwi kwayo na ni kule kuacha kitu cha wajibu pasi na udhuru wa Kishari´ah au udhuru wenye kuonekana au kuacha kitu kilichopendekezwa. Mfano wa aina ya kwanza ni kama mwanamke kuacha kuswali wakati yuko katika hedhi na mfano wa aina ya pili ni kama kuacha kuswali swalah ya adh-Dhuhaa´.

[1] Muslim (107). Hata hivyo matamshi haya yanapatikana kwa at-Twabaraaniy. al-Haythamiy na al-Mundhiriy wamesema:

”Wanaume wake ni wanaume sahihi.” (Majma´-uz-Zawaa-id (4/78) na at-Targhiyb)