36. I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuhusu Ujuu wa Allaah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Na katika yale tuliyotaja katika kumuamini Allaah, kunaingia kuamini yale Aliyoelezea Allaah katika Kitabu Chake, yaliyopokelewa kwa njia nyingi kutoka kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yale waliyokubaliana kwayo Salaf wa Ummah:

Ya kwamba Yeye (Subhaanah) Yuko juu ya mbingu Zake, juu ya ´Arshi yake na ametengana na viumbe Vyake. Na Yeye (Subhaanah) Yuko pamoja nao popote wanapokuwa na Anajua wanayoyafanya, kama Alivyojumuisha baina ya hayo katika Kauli Yake:

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

”Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akalingana juu ya ´Arshi. Anajua yanayoingia ardhini, na yatokayo humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo – Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah kwa myatendayo ni Mwenye kuyaona.” (57:04)

Na Kauli Yake “Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo haina maana ya kwamba Amechanganyika na viumbe Vyake. Lugha haidharurishi hilo na linakwenda kinyume na yale waliyokubaliana kwayo Salaf wa Ummah na linakwenda kinyume na umbile Aliloliumbia kwalo uumbaji. Mwezi ni Ishara katika Ishara za Allaah na ni katika Kiumbe Chake kidogo. Uko mbinguni daima na unakuwa pamoja na msafiri na asiyekuwa msafiri popote anapokuwa.

Na Yeye (Subhaanah) Yuko juu ya ´Arshi. Anaona viumbe Vyake, Anawalinda, Ana ujuzi juu yavyo na yasiyokuwa hayo katika maana ya Uola Wake. Maneno yote haya ambayo Allaah Ameyataja – ya kwamba Yuko juu ya ´Arshi na kwamba Yuko pamoja nasi – ni haki kwa uhakika wake na wala hayahitajii Tahriyf, lakini yanatakiwa kulindwa na misingi isiyokuwa na maana ya udanganyifu, kwa mfano kudhania ya kwamba udhahiri wa Kauli Yake “Fiys-Salmaa” (Mbinguni) maana yake kwamba Yuko mbinguni na mbingu ima inambeba au iko juu Yake. Hili ni batili kwa Ijmaa´ ya wanachuoni na watu wa Imani. Hakika ya Allaah, Kursiy Yake imeenea mbingu na ardhi na Yeye Ndiye Anayezuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Anazuia mbingu kwa Amri Yake Anafanya zisianguke kwenye ardhi isipokuwa kwa idhini Yake. Na ni katika Ishara Zake kusimama kwa mbingu na ardhi kwa Amri Yake:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ

“Na katika alama Zake, ni kwamba mbingu na ardhi zimesimama kwa amri Yake.” (30:25)

MAELEZO

Huu ni mlango muhimu sana katika kitabu hichi. Unaenda sambamba na yale yaliyotangulia katika kitabu. Anasema (Rahimahu Allaah):

“Na katika yale tuliyotaja katika kumuamini Allaah, kuamini kuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu ya mbingu, juu ya ´Arshi na ametengana na viumbe Vyake.”

Haya yamethibiti kwa dalili ya Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf wa Ummah. Salaf wa Ummah wote (Rahimahumu Allaah) ni wenye kuamini kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu ya mbingu zote na yuko juu ya ´Arshi na ametengana na viumbe Vyake.

Ametengana na viumbe Vyake – Maana yake ni kwamba hakuna kitu katika viumbe Vyake kilichoko kwenye dhati Yake na kadhalika hakuna kitu katika dhati Yake kilichoko kwenye viumbe Vyake. Ametengana nao. ´Abdullaah bin al-Mubaarak na wengineo wamesema:

“Tunamtambua Mola wetu ya kwamba yuko juu ya mbingu zote, juu ya ´Arshi Yake na ametengana na viumbe Vyake. Lakini elimu Yake iko kila mahali.”[1]

Kadhalika ndivyo wanavyosema Salaf wengine wote (Rahimahumu Allaah) ya kwamba Allaah (Subhaanah) yuko juu ya mbingu zote na juu ya ´Arshi na ujuzi Wake uko kila mahali. Hakuna mgongano kati ya ueneaji wa ujuzi Wake na kuwa Kwake juu. Hakika Yeye (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi na wakati huo huo ujuzi Wake uko kila mahali na umekizunguka kila kitu. Anakijua kila kitu. Ameoanisha hayo mawili katika maneno Yake (Subhaanah):

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ۖ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Je, huoni kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo mbinguni na yale yote yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa [watu] watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, na wala [hauwi mnong’ono wa] chini kuliko ya hivyo, na wala wa wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao popote watakapokuwa; kisha Atawajulisha kwa yale [yote] waliyoyatenda Siku ya Qiyaamah – hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi daima.” (58:07)

Ameanza Aayah hii kwa kutaja ujuzi na akaimalizia kwa kutaja ujuzi. Hiyo ni dalili yenye kuonyesha kuwa ujuzi sio Ujuu. Ujuzi Wake ni wenye kukizunguka kila kitu na ni jambo limethibiti kwa dalili ya Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf wa Ummah huu. Vilevile kuwa Kwake juu ya ´Arshi ni jambo limethibiti kwa dalili ya Qur-aan na Sunnah. Hakuna mgongano kati ya hayo mawili.

Na Yeye (Subhaanah) Yuko juu ya ´Arshi. Anaona viumbe Vyake, Anawalinda… – Inatakiwa kumtakasa na dhana mbovu kama mtu kufikiria kuwa mbingu inambeba, iko juu Yake au ni Mwenye haja nayo. Sivyo hivyo. Yeye ndiye ambaye amezisimamisha mbingu na ´Arshi. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا

“Hakika Allaah Anazuia mbingu na ardhi zisitoweke.” (35:41)

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ

“Na katika alama Zake ni kwamba: mbingu na ardhi zimesimama kwa amri Yake.” (30:25)

Viumbe vyote vimesimama kwa ajili Yake (Jalla wa ´Alaa). Yeye ndiye Mwenye kuvizuia, Yeye ndiye Mwenye kuviendesha na Yeye ndiye ameviumba. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu ya ´Arshi Yake na juu ya viumbe vyote.

Maneno yote haya ambayo Allaah Ameyataja – ya kwamba Yuko juu ya ´Arshi… – Kuhusu Yeye kuwa pamoja na sisi na kuwa Kwake juu ya ´Arshi ni haki juu ya uhakika wake. Ni jambo lisilohitajia kupotoshwa na wala isifikiriwe kuwa amechanganyika na viumbe Vyake kama wanavyosema Mu´tazilah, Jahmiyyah na mapote mengine yanayokanusha sifa za Allaah. Hakika (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi na ujuzi Wake uko kila mahali. Kwa msemo mwingine anakijua kila kitu kilicho mbinguni na ardhini.

Muumini anatakiwa kufuata ´Aqiydah hii kubwa iliyothibiti kwa Qur-aan na Sunnah. Hii ndio ´Aqiydah ambayo Salaf wa Ummah katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waliokuja baada yao wamekubaliana kwayo ya kwamba kitendo cha Allaah kuwa juu hakipingani na kuwa kwake pamoja na viumbe Vyake (al-Ma´iyyah) na kuwazunguka Kwake kiujuzi. Ujuu ni kitu na kukizunguka Kwake kila kitu kiujuzu ni kitu kingine. Hakuna chochote chenye kumpita katika elimu Yake, si mbinguni wala ardhini pamoja na kuwa yuko juu ya ´Arshi na juu ya viumbe vyote (Subhaanahu wa Ta´ala):


لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

“… ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni Muweza na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi Wake.” (65:12)

إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi.” (08:75)

إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Hakika Allaah juu ya kila kitu ni Muweza.” (02:20)

وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقْتَدِرًا

“Na Allaah daima juu ya kila kitu ni Mwenye Uwezo wa juu kabisa.” (18:45)

[1] Ameipokea ´Abdullaah bin Ahmad katika “as-Sunnah” (44), uk. 13, ad-Daarimiy katika “ar-Radd ´alaa al-Jahmiyyah” (67), uk. 47, Ibn Battwah katika “al-Ibaanah” (2528) (02/148).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com