Kufunga mwezi wa Ramadhaan ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na wa kike. Ni moja katika nguzo za Uislamu tena nguzo kubwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ

“Enyi walioamini! Mmefaradhishiwa kufunga.”[1]

Maana ya ´mmeandikiwa` bi maana mmefaradhishiwa.

Kwa hivyo msichana akifikisha umri wa uwajibu wa kufunga kwa kudhihiri moja katika zile alama za kubaleghe – moja katika alama ikiwa ni hedhi – basi ulazima wa kufunga utaanza juu yake. Anaweza kupata hedhi akiwa na miaka tisa. Huenda wakajahili baadhi ya wasichana kwamba ni lazima kwao kufunga katika kipindi hicho na hivyo akaacha kufunga kwa kufikiria kuwa ni mdogo na wala familia yake wasimwamrishe kufunga, jambo ambalo ni uzembeaji mkubwa kwa kuacha nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu. Aliyefikiwa na jambo hilo basi ni lazima kwake kulipa funga aliyoacha tangu pale alipoanza kupata hedhi hata kama kumeshapita muda mrefu. Kwa sababu bado ni yenye kubaki katika dhimma yake[2].

[1] 02:183

[2] Ni wajibu vilevile kwake – mbali na kulipa – kulisha masikini kwa kila siku moja iliyompita 1,5 kg ya chakula.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 85
  • Imechapishwa: 06/11/2019