35. Tafsiri ya Qur-aan kwa mujibu wa Ibn ´Abbaas

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba amesema:

“Qur-aan inafasiriwa kwa njia nne: tafsiri ambayo waarabu wanaielewa kupitia lugha yake, tafsiri ambayo hakuna yeyote anayepewa udhuru kwa kutoijua, tafsiri inayojulikana na wanachuoni na tafsiri ambayo hakuna anayeijua isipokuwa Allaah pekee; yeyote mwenye kudai kuijua, basi huyo ni mwongo.”

1- Tafsiri ambayo waarabu wanaielewa kupitia lugha yake ni maneno ya msamiati. Kwa mfano wa maana ya ada ya mwezi (القرء), mito (النمارق), pango (الكهف) na mfano wake.

2- Tafsiri ambayo hakuna yeyote anayepewa udhuru kwa kutoijua. Ni tafsiri ya zile Aayah ambazo ni lazima kuziamini na kuzitendea kazi. Kama kwa mfano kumtambua Allaah kwa majina na sifa Zake, kuwa na utambuzi juu ya Qiyaamah, wudhuu´, swalah, zakaah na mfano wa hayo.

3- Tafsiri inayojulikana na wanachuoni. Ni tafsiri ya zile Aayah ambazo ni zenye kufichikana kwa wengine. Kuna uwezekano wa kuzitambua kwa kule kutambua sababu ya kuteremka kwake, chenye kufuta na chenye kufutwa, kilichoenea na ambacho ni maalum, cha wazi na kisichokuwa wazi na mfano wa hayo.

4- Tafsiri ambayo hakuna anayeijua isipokuwa Allaah pekee. Ni ule uhakika wa yale ambayo Allaah amejielezea Mwenyewe na juu ya siku ya Mwisho. Tunafahamu maana ya mambo haya, lakini hatujui uhakika wa mambo yalivyo. Kwa mfano tunaelewa maana ya kwamba Allaah amelingana juu ya ´Arshi, hata hivyo hatujui namna ya uhalisia wake. Kadhalika tunaelewa maana ya matunda, asali, maji, maziwa na vyenginevyo ambavyo Allaah amesema kuwa viko Peponi. Lakini hata hivyo hatujui uhakika wa mambo yalivyo. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاء بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Hakuna yeyote anayejua yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho yakiwa ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[1]

Ibn ´Abbaas amesema:

“Hakuna kitu katika dunia hii kinachofanana na kilichoko Peponi isipokuwa kwa jina tu.”[2]

Mpaka hapa imebainika kuwa katika Qur-aan kuna Aayah ambazo hakuna anayejua tafsiri yake isipokuwa Allaah pekee. Mfano wa hilo ni uhakika wa majina, sifa Zake na yale aliyoelezea Allaah juu ya siku ya Qiyaamah. Kuhusu maana ya mambo haya, tunaijua. Vinginevyo kusingekuwa na maana yoyote ya kuyataja – na Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] 32:17

[2] Tazama ”az-Zuhd” (1/51/8) ya Hannaad na ”Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym” (1/64) ya Ibn Kathiyr.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 13/05/2020