35. Msimamo wa Ahl-us-Sunnah kwa Ahl-ul-Bayt na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh)

Aidha Ahl-us-Sunnah wanaonelea kuwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ni kama Maswahabah wengine wote, kwamba yeye ni khaliyfah wa nne ana fadhila zake na kwamba yeye ni mmoja miongoni mwa wale Maswahabah kumi waliobashiriwa Pepo. Pamoja na yote haya hawapitilizi kwake, hawamuombi pamoja na Allaah, hawasemi kuwa amekingwa na kukosea na wala hawasemi kuwa yeye ndiye alikuwa ni mwenye kustahiki utume na kwamba Jibriyl (´alayhis-Salaam) alifanya usaliti. Yote haya ni batili. Lakini wanaona kuwa ni miongoni mwa Maswahabah wabora na wema (Radhiya Allaahu ´anhum). Pamoja na yote haya hawavuki mipaka kwao, hawavuki mipaka kwa Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa), al-Hasan na al-Husayn (Radhiya Allaahu ´anhumaa) na wengineo. Bali wanaonelea kuwa yule mwenye kufuata haki miongoni mwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye ambaye ana sifa za waumini, anastahiki kuombewa na kutakiwa radhi. Lakini hata hivyo hawavuki mipaka kwao. Wanazitambua fadhila zao, kwamba wao ndio waislamu bora kabisa na wana nafasi yenye kujulikana mbele ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com