35. Miongoni mwa hukumu za twahara katika swalah


Swali 35: Utoko unaomtoka mwanamke – ni mamoja utoko huo ni mweupe au wa manjano – ni msafi au ni najisi? Unawajibisha kutawadha pamoja na kuzingatia kwamba ni kushuka nyakati zote? Ni ipi hukumu ikiwa ni wenye kushuka baadhi ya nyakati na khaswa wanawake wengi na mara nyingi wale wasomi wanazingatia kuwa ni unyevu wa kimaumbile usiomlazimu kutawadha?

Jibu: Kilichonidhihirikia mimi baada ya utafiti ni kwamba utoko unaomtoka mwanamke ikiwa hautoki kwenye kibofu cha mkojo bali unatoka kwenye kifuko cha uzazi basi ni msafi. Lakini unachengua wudhuu´ hata kama ni msafi. Kwa sababu kuchenguka kwa wudhuu´ hakushurutishi kitu kiwe cha najisi. Huu hapa upepo unatoka kupitia tupu ya nyuma na hauna athari. Licha ya hivo unachengua wudhuu´. Kujengea juu ya haya ukimtoka mwanamke ilihali yuko na wudhuu´ basi wudhuu´wake unachenguka na hivyo atalazimika kutawadha upya.

Ikiwa utoko huu ni wenye kutoka nyakati zote hauchengui wudhuu´. Lakini atatakiwa kutawadha kwa ajili ya swalah pindi utapoingia wakati wake na ataswali faradhi au swalah ya sunnah katika wakati huu ambapo ametawadha ndani yake. Pia inafaa kwake kusoma Qur-aan na mengine anayotaka miongoni mwa yale aliyoruhusiwa. Hivo ndivo walivosema wanachuoni juu ya mtu kama huyu ambaye anatokwatokwa na mkojo nyakati zote. Hii ndio hukumu ya utoko ni msafi.

Kuhusu kwamba unachengua wudhuu´ ni wenye kuchengua wudhuu´. Isipokuwa ikiwa ni wenye kumtoka nyakati zote. Ikiwa ni wenye kumtoka nyakati zote haichengui wudhuu´. Lakini mwanamke analazimika kutadha baada ya kuingia wakati na ajihifadhi vizuri.

Ikiwa utoko huo si wenye kutoka nyakati zote na ikawa miongoni mwa mazowea yake unakatika nyakati za swalah, basi atachelewesha swalah mpaka ule wakati ambao utoko umesita midhali hachelei kutoka nje kwa muda wa swalah. Akikhofia kumalizika kwa wakati wa swalah basi atatawadha, atajisitiri vizuri kwa kitambara na kuswali.

Hapana tofauti kati ya utoko mwingi na mdogo kwa sababu wote ni wenye kutoka kupitia njia hiyo. Kwa hivyo ni wenye kuvunja sawa ukiwa mdogo au mwingi. Tofauti na kile kinachotoka kupitia viungo vingine vya mwili kama mfano wa damu na matapishi. Vitu kama hivi havichengui wudhuu´ ni mamoja vitoke kidogo au kwa wingi.

Sijui msingi wa vile wanavyoonelea baadhi ya wanawake kwamba kwamba utoko hauchengui wudhuu´. Isipokuwa maoni ya Ibn Hazm (Rahimahu Allaah) ambaye anaona kuwa kitu hicho hakichengui wudhuu´. Pamoja na hivyo hakutaja dalili ya hilo. Angekuwa yuko na dalili kutoka katika Qur-aan, Sunnah au maneno ya Maswahabah basi ingelikuwa ni hoja.

Ni lazima kwa mwanamke kumcha Allaah na apupie juu ya twahara yake. Kwani hakika swalah haikubaliwi pasi na twahara licha ya kuwa mtu ataswali mara mia. Bali baadhi ya wanachuoni wanasema kuwa mwenye kuswali bila ya wudhuu´ anakufuru. Kwa sababu kufanya hivo ni katika kuzichezea shere Aayah za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 60 su-aal wa jawaab fiy Ahkaam-il-Haydhw, uk. 32-34
  • Imechapishwa: 31/07/2021