35. Kuamini kujitokeza kwa ad-Dajjaal


Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini kuwa al-Masiyh ad-Dajjaal atajitokeza. Kati ya macho yake kumeandikwa “kafiri”. Hadiyth zilizokuja juu ya hilo na kuamini kuwa hilo litakuwepo.

MAELEZO

Kumepokelewa Hadiyth nyingi Swahiyh juu ya hili. Kumepokelewa Hadiyth nyingi kuhusu kujitokeza kwa ad-Dajjaal na kuteremka kwa  ´Iysaa. Katika hizo ni Hadiyth mnayoisoma kila siku katika swalah zenu:

اللهم إني أعوذ بك من عذاب القبر، و من عذاب النار، و من فتنة المحيا و الممات، و من فتنة المسيح الدجال

“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda kwako kutokamana na adhabu ya kaburi, adhabu ya Moto, mtihani wa uhai na wa kifo na mtihani wa al-Masiyh ad-Dajjaal.”

Kwa masikitiko wako watu wanaopinga kujitokeza kwa ad-Dajjaal na wanapotosha maana yake. Moja katika upotoshaji wa ajabu ni kuwa si yeye wala ´Iysaa kwamba sio watu. Badala yake wanamaanisha kuwa inahusiana na mielekeo ya kiroho na ya pesa. Wanasema kuwa ad-Dajjaal ndiye mwelekeo wa kipesa na mwelekeo wa kiroho ndio ´Iysaa.

Kama tulivyosema kumepokelewa Hadiyth nyingi kuhusu ad-Dajjaal na kuteremka kwa ´Iysaa. Baadhi yazo zimepokelewa na Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Umar, Anas, Hudhayfah, Ibn Mas´uud na Abu Hurayrah. Kila Mtume alitahadharisha juu ya huyu ad-Dajjaal na vivyo hivyo ndivyo alivyofanya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi aliposema:

“Mimi nakutahadharisheni nae. Nitakuelezeni jambo ambalo hajakuelezeni yeyote kabla yangu: yeye hana jicho moja la kulia.”[1]

Ataonekana kama mwenye kuleta Pepo na Moto, mto kutoka Motoni na mto kutoka Peponi. Uhakika wa mambo mto kutoka Peponi ndio Moto na mto wa Motoni ndio Pepo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemwamrisha muumini atayekutana na haya ainamishe kichwa, afumbe macho yake na anywe kutoka kwenye ule mto unaoonekana kama Moto – kwani hakika ni maji ya baridi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi ni mjuzi zaidi wa yale atayokuja nayo ad-Dajjaal kuliko yeye mwenyewe anavyojua.”[2]

Mtume anajua zaidi kuliko ad-Dajjaal. ad-Dajjaal hajui kuwa mto wake huu kutoka Peponi uhalisia wake ni Moto na kwamba mto wake huu kutoka Motoni ni Pepo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametueleza ukweli. Ni moja katika miujiza yake inayothibitisha ukweli wa utume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Katika mnasaba wa kutajwa kwa ad-Dajjaal Maswahabah walisikia namna ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ananyanyua na kushusha sauti. Walipomuuliza sababu ya hilo akasema:

“Sio ad-Dajjaal ambaye mimi nachelea zaidi kwenu.”

Kwa sababu neno “kafiri” limeandikwa kwenye paji lake la uso. Kila muumini, sawa yule anayeweza kusoma na asiyeweza, wataisoma. Ni alama ya wazi kuwa ni kafiri tofauti na yule anayevaa mavazi ya Kiislamu, anazungumza kwa jina la Uislamu na anatumia nembo ya Uislamu. Mtu kama huyu madhara yake ni makubwa zaidi. Watatizi na waongo hawa ni wengi kwelikweli na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametutahadharisha nao.

[1] al-Bukhaariy (7127).

[2] Muslim (2934).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 402-403
  • Imechapishwa: 19/09/2017