36. Dalili ya khofu


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya khofu ni maneno Yake (Ta´ala):

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu na nikhofuni Mimi mkiwa ni waumini.” (Aal ´Imraan 03 : 175)

MAELEZO

Khofu ni mhemko anapata mtu wakati anaogopa kifo, madhara au maudhi. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amekataza kuwaogopa wapenzi wa shaytwaan na badala yake akaamrisha kumuogopa Yeye peke yake.

Khofu imegawanyika aina tatu:

1- Khofu ya kimaumbile. Mfano wa hilo ni mtu kuogopa wanyama wakali, moto na kuzama. Khofu kama hii mja hasemwi vibaya kwayo. Allaah (Ta´ala) Amesema kuhusu Muusa (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

فَأَصْبَحَ فِي الْمَدِينَةِ خَائِفًا يَتَرَقَّبُ

“Akapambaukiwa kuwa mwenye khofu katika mji ule anaangaza.” (al-Qaswasw 28 : 18)

Lakini endapo khofu kama hii itakuwa ni sababu ya kuacha jambo la wajibu au kufanya kitu cha haramu, kama alivyosema Shaykh (Rahimahu Allaah), basi khofu hii inakuwa haramu. Kila ambacho ni sababu ya kuacha kitu cha wajibu au kufanya jambo la haramu inakuwa ni haramu. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu na nikhofuni Mimi mkiwa ni waumini.”

Hata hivyo khofu ya kumuogopa Allaah (Ta´ala) wakati fulani inaweza kuwa yenye kusemwa vizuri na wakati mwingine inaweza kuwa yenye kulaumiwa.

Kuhusiana na khofu yenye kusemwa vizuri ni ile ambayo ikiwa lengo ni kutomuasi Allaah. Inapitika kwa kukufanya kutenda mambo ya wajibu na kuacha mambo ya haramu. Lengo hili likitimizwa, basi moyo hupata utulivu na unazidiwa na furaha kwa neema za Allaah na kutaraji thawabu Zake.

Ama kuhusu yenye kusemwa vibaya, ni ile inayomfanya mja kukata tamaa na reheme za Allaah. Matokeo yake mja hudhurika na kupata hasara. Vilevile huenda kutokana na ile nguvu ya kukata kwake tamaa ikampelekea kuzidi kuingia katika maasi zaidi.

2- Khofu ya ´ibaadah. Hili linapitika kwa mtu kufanya ´ibaadah kwa khofu. Aina hii hafanyiwi yeyote isipokuwa Allaah pekee. Kumfanyia mwingine asiyekuwa Allaah (Ta´ala) ni shirki kubwa.

3- Khofu ya siri. Kwa mfano mtu akamuogopa aliye ndani ya kaburi au walii aliye mbali na yeye na hawezi kumfanya lolote. Licha ya hivyo akawa anamuogopa kwa khofu ya siri. Wanachuoni wamesema kuwa hii pia ni shirki.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 57
  • Imechapishwa: 22/05/2020