Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika Hadiyth imekuja:

“Du´aa ndio kiini cha ´ibaadah.”

Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

“Na Mola wenu amesema: “Niombeni Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari na ‘ibaadah Yangu, watauingika Moto wa Jahanam wadhalilike.” (Ghaafir 40 : 60)

MAELEZO

Hapa mtunzi (Rahimahu Allaah) anaanza kutaja dalili ya aina za ´ibaadah ambazo amezitaja hapo nyuma. Ameanza (Rahimahu Allaah) kutaja dalili ya du´aa. Kuhusu upambanuzi wa dalili ya Uislamu, imani na ihsaan, zitakuja hapo mbele – Allaah akitaka.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) ametumia dalili yale yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Du´aa ndio kiini cha ´ibaadah.”

Vilevile ametumia dalili kwa maneno Yake (Ta´ala):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

“Na Mola wenu amesema: “Niombeni Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari na ‘ibaadah Yangu, watauingika Moto wa Jahanam wadhalilike.”

Aayah hii tukufu imefahamisha kwamba du´aa ni miongoni mwa ´ibaadah. Lau mambo yasingelikuwa hivo basi isingesihi kusema:

إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

“Hakika wale wanaotakabari na ‘ibaadah Yangu, watauingika Moto wa Jahanam wadhalilike.”

Hivyo basi, yule mwenye kumuomba mwingine asiyekuwa Allaah kwa kitu ambacho hakiwezi yeyote isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall), basi huyo ni mshirikina kafiri. Pasi na kujali sawa ikiwa huyu mwenye kuombwa bado yuhai au ameshakufa. Hata hivyo, mwenye kumuomba mtu ambaye yuhai kwa kitu ambacho anakiweza, kwa mfano akamuomba chakula au kinywaji, hakuna neno juu yake. Mwenye kumuomba mfu au kiumbe asiyekuwa mbele yako kwa kitu kama hicho, basi mtu huyu anazingatiwa kuwa ni mshirikina. Kwa sababu mfu au mtu asiyekuweko mbele yako hawezi akakufanyia kitu kama hichi. Kwa ajili hiyo maombi yake kwa watu hao ni dalili inayoonesha kuwa anaamini ya kwamba wanauendesha ulimwengu – na hili linamfanya kuwa ni mshirikina!

Tambua ya kwamba kuna aina mbili za du´aa; du´aa ya kuomba na du´aa ya ´ibaadah.

1- Du´aa ya kuomba inahusiana na kuomba kitu chochote, mtu akaomba haja zake. Aina hii inazingatiwa kuwa ni ya ´ibaadah ikiwa mja anamuomba Mola Wake. Kwa kuwa kitendo hichi ndani yake kuna kujidhalilisha kwa Allaah (Ta´ala) na kumtegemea Yeye. Kadhalika kinaonyesha kwamba anaonelea kuwa Allaah ni Muweza, Mkarimu, Mwenye fadhilah na rehema kunjufu. Vilevile inajuzu du´aa kama hii mja akamuomba kiumbe mwenzake, muda wa kuwa muombwaji huu anafahamu maombi haya na akawa na uwezo wa yale anayoombwa, kama ilivyotangulia kusema mtu akamuomba mwengine chakula.

2- Kuhusu du´aa ya ´ibaadah, inahusiana na kumwabudu yule anayeombwa, hali ya kutarajia thawabu zake na kuogopa adhabu zake. Hii haisihi kufanyiwa asiyekuwa Allaah. Kumfanyia aina hii asiyekuwa Allaah ni shirki kubwa inayomtoa mtu nje ya Uislamu. Vilevile anaingia katika matishio ya maneno Yake (Ta´ala):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

“Na Mola wenu amesema: “Niombeni Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari na ‘ibaadah Yangu, watauingika Moto wa Jahanam wadhalilike.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 55-56
  • Imechapishwa: 22/05/2020