35. Dalili kutoka katika Sunnah juu ya kuthibiti kwa majina na sifa za Allaah

2- Miongoni mwa dalili juu ya kuthibiti majina ya Allaah kutoka katika Sunnah zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni yale yaliyopokea Abu Hurayrah ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah ana majina tisini na tisa – mia moja kasoro moja. Yule atakayeyadhibiti ataingia Peponi.”[1]

Majina ya Allaah hayakufupika kwa idadi hii. Dalili ya hilo ni yale aliyopokea ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninakuomba kwa kila jina ambalo ni Lako, umejiita kwalo nafsi Yako, umeliteremsha katika Kitabu Chako, umemfunza mmoja katika viumbe Wako au umelificha katika elimu ya ghaibu huko Kwako uijaalie Qur-aan tukufu iwe ni nguvu ya moyo wangu… “[2]

Kila jina miongoni mwa majina ya Allaah limebeba sifa miongoni mwa sifa Zake. Kwa mfano Mjuzi wa kila kitu (al-´Aliym) linafahamisha ujuzi, Mwingi wa hekima (al-Hakiym) linafahamisha hekima, Mwenye kusikia kila kitu (as-Samiy´) na Mwenye kuona kila kitu (al-Baswiyr) yanafahamisha kusikia na kuona. Kila jina linafahamisha sifa miongoni mwa sifa za Allaah (Ta´ala). Amesema (Ta´ala):

قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ اللَّهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Sema: “Yeye ni Allaah – Mmoja pekee, Allaah aliyekamilika, mkusudiwa wa haja zote. Hakuzaa na wala hakuzaliwa, na wala hakuna yeyote anayefanana na kulingana Naye.”[3]

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba:

“Kuna mtu mmoja kutoka katika Answaar ambaye alikuwa akiwaswalisha katika msikiti wa Qubaa´. Basi ikawa kila anapoanza Suurah basi haunza kwa “Qul huwa Allaahu ahad” mpaka aimalize kisha ndio anasoma Suurah nyingine. Alikuwa akifanya hivo katika kila Rak´ah. Wenzake wakamsemeza na kumwambia: “Hakika wewe unaanza kwa Suurah hii kisha huoni kuwa inakutosha mpaka usome nyingine; ima uisome au uiache na usome nyingine.” Akasema: “Mimi si mwenye kuiacha. Mkipenda niwaswalishe namna hiyo sawa na mkichukia basi nitakuacheni.” Walikuwa wanamuona yeye ndiye mbora wao na wakachukia kuswalishwa na mwengine. Walipoenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumpa khabari akasema: Ee fulani! Ni kipi kinachokuzuia kufanya wanachokuamrisha marafiki zako na ni kipi kinachokufanya kulazimiana na Suurah hii katika kila Rak´ah?” Akasema: “Mimi naipenda.” Akasema: “Kuipenda kwako kumekuingiza Peponi.”[4]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtuma mtu katika kikosi na alikuwa akiwasomea wenzake katika swalah yao na akimalizia kwa “Qul huwa Allaahu ahad”. Waliporudi wakamweleza hayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Muulizeni ni kwa nini anafanya kitu hicho?” Walipomuliza akasema: “Ni kwa sababu ni sifa ya Mwingi wa huruma na mimi napenda kuisoma.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mwelezeni kuwa Allaah (Ta´ala) anampenda.”[5]

Bi maana imekusanya sifa za Mwingi wa rehema.

Yeye (Subhaanah) ameeleza kuwa ana uso. Amesema:

وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ

“Utabakia uso wa Mola wako wenye utukufu na ukarimu.”[6]

kwamba ana mikono miwili. Amesema:

مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

”Kipi kilichokuzuia usimsujudie niliyemuumba kwa mikono Yangu?”[7]

بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ

“Bali mikono Yake imefumbuliwa.”[8]

Kwamba anapenda, anachukia, anaghadhibika na anachukia. Zipo sifa nyingi ambazo Allaah amejisifu nazo au Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemsifu kwazo.

[1] al-Bukhaariy (2736) na Muslim (6751).

[2] Ahmad (3712).

[3] 112:01-04

[4] al-Bukhaariy (774).

[5] Ibn Jariyr at-Twabariy katika tafsiri yake ”Jaamiy´-ul-Bayaan” (16/446).

[6] 55:27

[7] 38:75

[8] 05:64

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 66-67
  • Imechapishwa: 02/03/2020