35. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya kushuka kwa Allaah

Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

وقل ينزلُ الجبارُ في كلِّ ليلةٍ

11 – Sema “al-Jabbaar hushuka katika kila usiku

بلا كيفَ جلَّ الواحدُ المُتمَدحُ

     pasi na namna – Ametukuka Mmoja mwenye kuhimidiwa”

MAELEZO

Anamzungumzisha Sunniy ambaye ameshikamana na Qur-aan na Sunnah. Sema na wala usiteteleki.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“al-Jabbaar hushuka… “

Allaah (Jalla wa ´Alaa) hushuka katika mbingu ya dunia kila usiku.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“… katika kila usiku.”

Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye kasema hivo. Yeye ndiye mjuzi zaidi kumtambua Mola Wake na yanayolingana Naye. Sema aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mthibitishie Allaah kushuka.

Kushuka ni katika sifa Zake za kimatendo ambazo anazifanya (Jalla wa ´Alaa) kwa utashi na matakwa Yake pale anapotaka. Kushuka huku kumepokelewa kwa mapokezi tele ya Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wamezipokea kundi kubwa la Maswahabah na ziko katika vitabu “as-Swahiyh”. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu cha kipekee akifafanua Hadiyth ya kushuka. Kitabu hicho kimechapishwa kipekee na kadhalika kimechapishwa pamoja na “Majmuu´-ul-Fataawaa”. Anwani yake ni “Sharh Hadiyth-in-Nuzuul”.

Ni wajibu kuthibitisha kushuka kama alivyothibitisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hushuka kila usiku pale kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku. Haya yanawasambaratisha wakanushaji. Kwa kuwa yamepokelewa kwa mapokezi mengi. Wamezowea kusema kuwa Hadiyth imesimuliwa na mpokezi mmoja na kwamba haifidishi elimu. Lakini hapa hawana namna kwa kuwa zimepokelewa Hadiyth tele kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kushuka huku ni kama sifa Zake zingine (Jalla wa ´Alaa). Sio kama kushuka kwa viumbe. Ni kushuka kwa al-Jabbaar (Jalla wa ´Alaa) ambako kunalingana na utukufu Wake. Hatujui namna yake. Sisi tunathibitisha kama ilivyokuja na hali ya kuwa tunaamini hilo. Hatuipindishi maana, hatuikanushi na wala hatuifananishi na kushuka kwa viumbe. Ni kushuka kunakolingana na ukubwa wa Allaah (Jalla wa ´Alaa).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 96-97
  • Imechapishwa: 09/01/2024