35. Allaah ni Mwenye kufanya akitakacho na hakukuwi kitu ila akitakacho


Baada ya hapo (Rahimahu Allaah) akasema:

“Naamini kuwa Allaah ni Mwenye kufanya Akitakacho.”

Haya ni masuala mengine. Nayo ni kuhusiana na kuamini matendo ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Yeye ana majina, sifa, matendo na matakwa na utashi:

“faalun lima yurid”

Anaumba, anaruzuku, anahuisha, anafisha na anaendesha mambo. Haya ni matendo ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Yeye kwa matakwa na utashi Wake (Subhaanahu wa Ta´ala):

فَعَّالٌ لِّمَا يُرِيدُ

“Mwingi wa kufanya Atakalo.”[1]

إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ

“Hakika Allaah anafanya atakavyo.”[2]

وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ

“Lakini Allaah anafanya ayatakayo.”[3]

Anafanya ayatakayo na anafanya akipendacho. Maneno yake:

“Hakukuwi kitu isipokuwa kwa kutaka Kwake.”

Yanayokuwa katika ulimwengu huu ni kutokana na uumbaji Wake (Subhaanahu wa Ta´ala), matakwa na utashi Wake. Hakukuwi katika ulimwengu huu chochote pasi na matakwa Yake na uumbaji Wake na kwamba hakuna yeyote anayeumba pamoja na Allaah. Hapa kuna Radd kwa Mu´tazilah wanaosema kuwa mja anajiumbia matendo yake mwenyewe na kwamba hakuumba matendo ya waja na kwamba wao wenyewe ndio wamejiumbia nayo hali ya kujitegemea kutokamana na Allaah (´Azza wa Jall). Wanaona kuwa Allaah hana matakwa wala utashi katika matendo hayo. Sisi tunaamini kuwa matendo ya waja ni uumbaji wa Allaah na ni chumo la waja. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah amekuumbeni pamoja na vile mnavovifanya.”[4]

 Bi maana ameumba pia yale myafanyayo.

[1] 85:16

[2] 22:18

[3] 02:253

[4] 37:96

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 55-56
  • Imechapishwa: 18/03/2021