Zakir Naik amesema:

“Je, Allaah Anaweza kuumba kila kitu? Wengi watasema “ndio”. Je, Allaah Anaweza kuharibu kila kitu? Wengi watasema “ndio.” Swali langu la tatu ni “Je, Allaah Anaweza kuumba kitu ambacho hawezi kukiharibu?” Wanatumbukia kwenye mtego. Ikiwa watasema “Ndio” itakuwa inaenda kinyume na jibu la pili, nalo kwamba Allaah Hawezi kuharibu kila kitu. Na ikiwa watasema “Hapana” itakuwa inaenda kinyume na jibu la kwanza, nalo kwamba Allaah Hawezi kuumba kila kitu. Ni kama tulivyosema wanatumia mantiki na wakatumbukia kwenye mtego. Kwa njia hiyo hiyo Allaah Hawezi Kuumba mtu ambaye ni mrefumfupi. Ni kweli Anaweza Kuumba mtu mrefu akawa mfupi, lakini atakuwa sio tena mrefu. Na Anaweza Kuumba mtu mfupi akawa mrefu, lakini atakuwa sio tena mfupi. Mtu hawezi kuwa mfupi na mrefu kwa wakati mmoja. Hata hivyo anaweza kuwa wa kati na kati, bi maana sio mrefu wala mfupi. Allaah Hawezi Kuumba mtu ambaye ni mrefu na wakati huo huo akawa ni mfupi. Hali kadhalika Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Hawezi Kuumba mtu mnenemwembamba. Ninaweza kukwambia maelfu ya vitu ambavyo Allaah Hawezi kufanya.”

Swali: Kuna mlinganiaji anayejulikana ana ulinganizi wa ulimwengu. Anasema kwamba Allaah Hawezi kila kitu na kwamba anajua mambo 1000 ambayo Allaah (Ta´ala) Hawezi. Je, huyu anazingatiwa kuwa ni katika walinganiaji wanaolingania katika milango ya Motoni? Je, ni wajibu kutahadharisha watu naye?

Jibu: Huyu ni Mulhid (mkanamungu). Mwenye kusema maneno haya anakufuru Majina na Sifa za Allaah:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

”Na Allaah Ana Asmaaul-Husnaa (Majina Mazuri kabisa), basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaopotoa (kwa kuharibu utukufu, kukanusha, kugeuza maana, kushabahisha) katika Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.” (07:180)

إِنَّ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي آيَاتِنَا لَا يَخْفَوْنَ عَلَيْنَا ۗ أَفَمَن يُلْقَىٰ فِي النَّارِ خَيْرٌ أَم مَّن يَأْتِي آمِنًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ ۖ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

”Hakika wale wanaozipotosha Aayah Zetu hawatufichikii (Tunawaona na Tunawaelewa vyema). Je, basi yule atakayetupwa katika moto ni bora au yule atakayekuja akiwa katika amani Siku ya Qiyaamah? Tendeni mpendavyo; hakika Yeye kwa myatendayo ni Baswiyr(Mwenye kuyaona daima).” (41:40)

Anayesema kwamba Allaah sio Muweza juu ya kila jambo… Ametakasika Allaah. Allaah Anasema:

وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Na Allaah juu ya kila kitu ni Muweza.” (02:284)

Ni Aayah ngapi Allaah Anasema:

وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Na Allaah juu ya kila kitu ni Muweza.” (02:284)

وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرً

“Na Allaah daima juu ya kila kitu ni Muweza.” (33:27)

Allaah Hakuwekea mpaka uwezo wa kiungu. Ni Mutlaq (isiyo na mipaka) na inakusanya kila kitu. Ni Muweza juu ya kila kitu. Ni Mjuzi juu ya kila jambo. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Hakuwekea mpaka. Wewe ndiye unawekea mpaka na kusema kwamba kuna mambo ambayo Allaah Hajui na wewe ndio utakuwa unayajua? Huku ni kuharibu Majina na Sifa za Allaah. Sio walinganiaji wote wanaokuwa juu ya haki. Sikiliza maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kutakuwepo walinganiaji wanaolingania katika milango ya Motoni.”

Sio walinganiaji wote wanaokuwa juu ya haki.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/ftn–1432-08-22.mp3
  • Imechapishwa: 20/05/2018