26- Watu kumzungumza vyema maiti kutoka katika mkusanyiko wa waislamu ambao ni wakweli wasiopungua wawili wanaotokamana na majira zake wanaomtambua miongoni mwa watu wema na wasomi ni jambo linalomuwajibishia Pepo – kwa fadhilah za Allaah. Kuhusu hilo zipo Hadiyth kadhaa:

1- Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Kuna jeneza lilipitishwa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo likasifiwa kheri. [ndimi zengine zikafuatilia kumtaja kwa kheri]. [Wakasema: “Alikuwa – kutokana na tunavyojua – akimpenda Allaah na Mtume Wake]. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Imewajibika, imewajibika, imewajibika. Likapita jeneza lingine na likasemwa vibaya [ndimi zengine zikafuatilia kumtaja kwa ubaya]. [Wakasema: “Alikuwa muovu katika dini ya Allaah]. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Imewajibika, imewajibika, imewajibika.” ´Umar akasema: “Namtoa fidia baba yangu na mama yangu. Kumepitishwa jeneza na likasemwa vizuri ambapo ukasema: “Imewajibika, imewajibika, imewajibika.” Likapitishwa jeneza lingine na likasemwa kwa ubaya mbapo ukasema: “Imewajibika, imewajibika, imewajibika?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Yule ambaye mnamsifia kheri basi Pepo imemthubutikia kwake na yule ambaye mnamsifia uovu Moto umemthubutikia kwake. [Malaika ni mashahidi wa Allaah juu mbinguni] na nyinyi ni mashahidi wa Allaah ardhini. Nyinyi ni mashahidi wa Allaah ardhini. Nyinyi ni mashahidi wa Allaah ardhini. [Katika upokezi mwingine imekuja: “Waumini ndio mashahidi wa Allaah ardhini]. [Hakika Allaah ana Malaika wanaotamka kwa ndimi za wanaadamu juu ya ile kheri na shari iliyoko kwa mtu].”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/177-178, 05/192-193), Muslim (03/53), an-Nasaa´iy (01/273), at-Tirimidhiy (02/158) na ameifanya kuwa Swahiyh. Vilevile ameipokea Ibn Maajah (01/454), al-Haakim (01/377), at-Twayaalisiy (2062), Ahmad (03/179, 186, 197, 211, 245, 281) kupitia njia kutoka kwa Anas na mtiririko ni wa Muslim. Upokezi mwingine ni wa Ibn Maajah. Upokezi mwingine ni wa Ahmad na al-Bukhaariy. Ziada zote, isipokuwa kabla ya ile ya mwisho, ni za Ahmad na al-Bukhaariy. al-Bukhaariy amepokea sehemu katika ile ziada ya mwanzo, al-Haakim amepokea ziada ya mwisho na ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Mambo ni kama alivosema.

Ameipokea vilevile Abu Daawuud (02/72), an-Nasaa´iy, Ibn Maajah na at-Twayaalisiy (2388), Ahmad (02/261, 466, 470, 498, 528) kupitia njia mbili kutoka kwa Abu Hurayrah. Ziada ya mwisho ni ya an-Nasaa´iy ambaye amepokea kutoka kwake. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Njia nyingine cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

2- Abul-Aswad ad-Diyliy amesema:

“Nilifika al-Madiynah na yamejitokeza maradhi fulani na wao walikuwa wanakufa kifo kibaya. Nikaketi jirani na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Mara kukapitishwa jeneza na likasifiwa kheri ambapo ´Umar akasema: “Imewajibika.” Nikasema: “Ni kipi kumewajibika, ee kiongozi wa waumini?” Akajibu: “Nimesema kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna muislamu yeyote ambaye atashuhudiliwa kheri na wanne isipokuwa Allaah atamwingiza Peponi.” Tukasema: “Vipi wakiwa watatu?” Akasema: “Na waatatu.” Tukasema: “Vipi wakiwa wawili?” Akasema: “Na wawili.” Halatu hatukumuuliza kuhusu mtu mmoja.”

Ameipokea al-Bukhaariy, an-Nasaa´iy, at-Tirmdihiy na al-Bayhaqiy (04/75) ameisahihisha. Vilevile imepokelewa na at-Twayaalisiy (nambari. 23) na Ahmad (nambari. 129 na 204).

3- “Hakuna muislamu yeyote anayekufa ambapo akashuhudiliwa na wanne miongoni mwa watu wenye nyumba zilizokuwa jirani naye za karibu ya kwamba hawajui kutoka kwake chochote isipokuwa kheri isipokuwa Allaah (Ta´ala wa Tabaarak):

“Nimekubali maneno yenu.”

au atasema:

“Nimekubali ushahidi wenu na nimemsamehe yale msiyoyajua.”

Tambua kwamba mkusanyiko wa Hadiyth hizi tatu zinafahamisha kwamba ushuhuda huu si jambo lenye kuwahusu Maswahabah peke yao.  Bali ni jambo linawahusu pia wale waliokuja baada yao miongoni mwa waumini ambao wako katika njia yao katika imani, elimu na ukweli. Hayo ndio yaliyosemwa kwa njia ya kukata na al-Haafidhw Ibn Hajar katika “al-Fath”. Kwa hivyo yule anayetaka ubainifu zaidi arejee maneno yake.

Jengine ni kwamba kufungamanisha ushahidi wa watu wanne katika Hadiyth ya tatu kilicho dhahiri ni kwamba ni jambo lilikuwa kabla ya Hadiyth ya ´Umar ilio kabla yake. Ndani yake kuna kutoshelezeka na ushahidi wa watu wawili, na ndio nguzo tunayoitegemea.

Tumesema haya. Ama maneno yanayosemwa na watu punde tu baada ya kumaliza kuswali swalah ya janeza: “Mnamshuhudilia nini? Mtoleeni ushahidi wa kheri” halafu wanajibu kwa kusema: “mwema, ni miongoni mwa watu wa kheri na mfano wa maneno kama hayo” sio makusudio ya Hadiyth kabisa kabisa. Bali hiyo ni Bid´ah mbaya. Kwa sababu hayakuwa ni miongoni mwa matendo ya Salaf. Jengine ni kwa kuwa wale wanaomtolea ushuhuda mara nyingi hawajui hali ya yule maiti. Bali wakati mwingine wanaweza kushuhudilia kinyume na vile wanavyojua kwa sababu tu ya kutaka kuitikia matakwa ya yule anayeomba kumtolea ushuhuda wa kheri kwa kudhania kwao kwamba kitendo hicho eti kinamfaa maiti na kujahili kwao kuwa ushahidi wenye kunufaisha ni ule unaokwenda sambamba na uhalisia wa yule anayetolea ushahidi. Hayo ndio yanafahamishwa na maneno yake katika Hadiyth ya kwanza:

“Hakika Allaah ana Malaika wanaotamka kwa ndimi za wanaadamu juu ya ile kheri na shari iliyoko kwa mtu.”

Ameipokea Ahmad (03/242), Ibn Hibbaan (749- al-Mawaarid), al-Haakim (01/378) ambaye amesema:

“Swahiyh juu ya sharti za Muslim.”

na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

Vilevile iko na Hadiyth nyingine inayoitolea ushahidi ya Abu Hurayrah.

Ameipokea pia Ahmad (02/408). Ndani yake yumo Shaykh katika wanachuoni ambaye hakutajwa jina. Mpokezi aliyepokea kutoka kwake ni ´Abdul-Humayd bin Ja´far az-Ziyaadiy na sikupata wasifu wake.

Pia ina Hadiyth nyingine yenye kuitolea ushahidi ambayo ni Mursal kutoka kwa Bishr bin Ka´b.

Ameipokea Abu Muslim al-Kajjiy, kama ilivyo katika “al-Fath” (03/179).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 60-62
  • Imechapishwa: 13/02/2020