34. Uzindushi juu ya neno “tafsiri” (التأويل)

Kumetangulia kwamba tafsiri (التأويل) inaweza kuwa na maana tatu:

1- Tafsiri ikiwa na maana ya kuweka wazi na kuibainisha ile maana. Hii ni istilahi ya wafasiri wengi wa Qur-aan. Mfano wa hilo ni du´aa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akimuombea Ibn ´Abbaas:

“Ee Allaah! Mpe ufahamu aweze kuielewa dini na mfunze tafsiri.”[1]

Hili ni jambo lenye kujulikana kwa wanachuoni inapokuja katika Aayah za sifa na nyenginezo.

2- Uhakika wa linavyoishilia jambo. Hii ndio maana inayojulikana ya tafsiri iliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah. Allaah (Ta´ala) amesema:

هَلْ يَنظُرُونَ إِلاَّ تَأْوِيلَهُ

“Je, wanangojea nini isipokuwa matokeo yake?”[2]

ذَلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلاً

“Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[3]

Aayah za kuhusu sifa zinapofasiriwa kwa maana hii, kinachokusudiwa ni ile maana na uhakika wazo. Tafsiri hii hakuna aijuaye isipokuwa Allaah pekee.

3- Mtu kulipindisha andiko kutoka katika udhahiri wake na kwenda katika maana inayotofautiana na udhahiri wake. Hii ni istilahi ya wanafalsafa na wengineo waliokuja nyuma. Tafsiri hii imegawanyika aina mbili; ilio sahihi na isiyokuwa sahihi.

Ilio sahihi ni ile inayosapotiwa na dalili. Kwa mfano kufasiri maneno ya Allaah (Ta´ala):

فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ

“Unaposoma Qur-aan, basi omba kinga kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyefukuzwa.”[4]

Bi maana unapotaka kusoma Qur-aan.

Isiyokuwa sahihi ni ile isiyosapotiwa na dalili. Kwa mfano kufasiri Allaah kulingana juu ya ´Arshi kwamba ni kutawala juu ya ´Arshi, kwamba mkono wa Allaah maana yake ni nguvu Zake au neema Zake na mfano wa hayo.

[1] al-Bukhaariy (143) na Muslim (2477).

[2] 07:53

[3] 04:59

[4] 16:98

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 84
  • Imechapishwa: 13/05/2020