Maana ya Uislamu kilugha ni kunyenyekea. Maana ya Uislamu Kishari´ah ni mja kujisalimisha kwa Allaah kidhahiri na kindani kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Haya yanajumuisha dini yote. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلاَمَ دِينًا

“Nimeridhia Uislamu iwe ndio yenu.”[1]

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللّهِ الإِسْلاَمُ

“Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.”[2]

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الإِسْلاَمِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake.”[3]

Maana ya imani kilugha ni kusadikisha. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا أَنتَ بِمُؤْمِنٍ لِّنَا وَلَوْ كُنَّا صَادِقِينَ

“Nawe hutotuamini japo tukiwa ni wakweli.”[4]

Maana ya imani Kishari´ah ni kukiri kwa moyo kunakolazimisha maneno na vitendo. Hivyo imani ni kuamini kwa moyo, kutamka kwa ulimi na vitendo vya viungo. Dalili yenye kuonyesha kuwa vyote hivi vinaingia ndani ya imani ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Imani ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Mwisho na Qadar ya kheri na shari yake.”[5]

“Imani ni tanzu sabini na kitu. Ya juu yake kabisa ni neno “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” na ya chini yake ni kuondosha chenye kuudhi njiani. Hayaa ni tanzu pia ya imani.”[6]

Kumuamini Allaah na Malaika Wake na kadhalika ni kuamini kwa moyo.

Kusema “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ni kutamka kwa ulimi.

Kuondosha chenye kuudhi njiani ni vitendo vya viungo.

Kuwa na hayaa ni kitendo cha moyo.

Kwa hivyo inapata kujulikana kuwa imani inajumuisha dini yote. Basi hakuna tofauti kati ya Uislamu na imani pale yanapotajwa kwa kutenganishwa. Ama vikitajwa vyote viwili kwa pamoja, Uislamu unafasiriwa kuwa ni kujisalimisha kidhahiri ambapo ndani yake mna kutamka kwa ulimi na vitendo vya viungo vya mwili. Uislamu huu unatoka kwa muumini aliye na imani kamilifu na muumini aliye na imani dhaifu. Allaah (Ta´ala) amesema:

قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا قُل لَّمْ تُؤْمِنُوا وَلَكِن قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ

“Mabedui wa kiarabu walisema: “Tumeamini.” Waambie: “[Bado] hamjaamini – lakini semeni: “Tumesilimu!” Kwani imani haijaingia bado nyoyoni mwenu.”[7]

Uislamu huuhuu unaweza kutoka kwa mnafiki. Hata kama atakuwa ni muislamu kwa dhahiri, kwa ndani ni kafiri.

Katika hali hii imani inafasiriwa kuwa ni kujisalimisha kwa ndani ambapo kunaingia kukubali na kitendo cha moyo. Imani kama hii haitoki isipokuwa kwa muumini wa kweli. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا

“Hakika si vyenginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake basi huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea. Ambao wanasimamisha swalah na hutoa sehemu ya vile Tulivyowaruzuku; – hao ndio waumini wa kweli.”[8]

Katika hali hii imani inakuwa juu. Kwa hivyo kila muumini ni muislamu na si kinyume chake.

[1] 05:03

[2] 03:19

[3] 03:85

[4] 12:17

[5] al-Bukhaariy (50) na Muslim (9).

[6] al-Bukhaariy (9) na Muslim (35).

[7] 49:14

[8] 08:02-04

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 91-92
  • Imechapishwa: 13/05/2020