5 – Uharamu wa wanawake kuyatembelea makaburi. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Ni jambo linalotambulika kuwa mwanamke akifunguliwa mlango huu basi itampeleka katika kulalamika, kulia na kuomboleza kutokana na alivyo mdhaifu, malalamiko mengi na uchache wa subira. Pia hayo ni sababu inayomfanya yule maiti kuadhibiwa kwa kilio chake na wanaume kufitiniwa na sauti yake na sura zake, kama ilivyokuja katika Hadiyth nyingine “Hakika nyinyi mnawatia mitihanini waliohai na mnawaudhi maiti.” Ikiwa wanawake kuyatembelea makaburi ni sababu inayopelekea katika mambo ya haramu juu yao na juu ya wanaume – na hekima hapa haikudhibitiwa – basi haiwezekani kukakisiwa kiwango kisichoweza kupelekea katika hayo wala kupambanua kati ya aina hii na ile. Miongoni mwa misingi ya Shari´ah ni kwamba hekima ikiwa imejificha au si yenye kuenea, basi hukumu itafungamanishwa na sababu yake. Hivyo mlango huu utaharamishwa kwa kuziba njia. Ni kama ilivyoharamishwa kutazama mapambo ya ndani kutokana na ile fitina inayopelekea huko na kama ilivyoharamishwa kukaa faragha, mwanamke wa kando na mitazamo miengineyo. Wala hakuna katika hayo – yaani mwanamke kuyatembelea makaburi – manufaa isipokuwa kumuombea du´aa maiti, jambo ambalo anaweza kulifanya nyumbani kwake.”[1]

6 – Uharamu wa maombolezo. Kuomboleza ni kunyanyua sauti kwa kulalamika, kupasua nguo, kujipiga mashavu, kunyoa nywele, kuutia uso rangi nyeusi na kuuchanachana kwa ajili ya kumsikitikia yule maiti na kujiombea maangamivu na yasiyokuwa hayo katika mambo yanayofahahamisha kutoridhia mipango na makadirio ya Allaah na kutokuwa na subira. Kitendo hicho ni haramu na dhambi kubwa. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si katika sisi yule mwenye kujipiga kwenye mashavu, kuchana nguo na akatamka matamshi ya kipindi cha kishirikina.”

Wawili hao wamepokea tena kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amejitenga mbali na mwanamke mwenye kunyanyua sauti, mwenye kunyoa nywele zake na mwenye kupasua nguo zake.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamke mwenye kuomboleza na mwenye kusikiliza. Bi maana yule aliyekusudia kusikiliza maombolezo na akapendekezwa nayo.

Ee dada wa Kiislamu! Ni lazima kwako kujiepusha na kitendo hichi cha haramu wakati wa msiba. Ni wajibu kwako vilevile kusubiri na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah ili uweze kusamehewa madhambi yako na kuongezewa mema yako. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Wabashirie wenye kusubiri. Wale ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[2]

Inafaa kulia kilio ambacho ndani yake hakina maombolezo, matendo ya haramu wala kukasirika juu ya mipango na makadirio ya Allaah. Kwa sababu kulia kunaonyesha kumuhurumia maiti na ulaini wa moyo. Jengine ni kwamba ni miongoni mwa mambo ambayo mtu hawezi kuyazuia. Hivyo ndio maana ikaruhusiwa na pengine ikapendekezwa.

[1] (24/335-356).

[2] 02:155-157

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 69
  • Imechapishwa: 06/11/2019