34. Sifa na majina ya Allaah yaliyothibiti katika Sunnah IV

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah Ndiye Mola wa mbingu hizi saba na ardhi na Ndiye Mola wa ´Arshi kubwa. Mola Wetu na Mola wa kila kitu. Mpasuaji wa mbegu na kokwa na Ambaye Umeteremsha Tawraat, Injiyl na Qur-aan. Najikinga Kwako na shari ya nafsi yangu na shari ya kila kiumbe kiovu ambacho wewe una utawala juu yake. Wewe ni wa Mwanzo na hakuna kabla Yako kitu. Na Wewe ni wa Mwisho na hakuna baada Yako kitu. Na Wewe ni wa Juu na hakuna juu Yako kitu. Na wewe ni wa Karibu na hakuna kinachojifichika Kwako. Nilipitie deni langu na nitajirishe na ufakiri wangu.”[1]

Na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia Maswahabah pindi waliponyanyua sauti zao kwa Dhikr:

“Enyi watu! Zihurumieni nafsi zenu! Kwani hakika hamumuombi ambaye ni kiziwi wala asiyekuwepo. Hakika Yule mnayemwomba ni Mwenye Kusikia Mwenye kuona na Aliye karibu. Hakika yule mnayemwomba Yuko karibu na mmoja wenu kuliko shingo ya mpando wenu.”[2]

“Hakika nyinyi mtamuona Mola Wenu kama mnavyouona mwezi usiku wa mwezi mng’aro – hamtosongamana katika kumuona. Hivyo ikiwa mnaweza kuswali kabla ya jua kuchomoza na jua kuzama, basi fanyeni hivyo.”[3]

Tazama Hadiyth hizi na mfano wake ambapo anaelezea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Mola Wake. Hakika al-Firqat-un-Naajiyah, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, wanaamini hayo kama jinsi wanavyoamini Aliyojielezea Allaah katika Kitabu Chake, bila ya Tahriyf, Ta´twiyl, Takyiyf wala Tamthiyl.

Bali wao wako kati kwa kati baina ya mapote ya Ummah, kama jinsi Ummah ulivyo kati kwa kati baina ya Ummah zingine.

Wako kati kwa kati katika mlango wa Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) – baina ya Ahl-ut-Ta´twiyl wanaokanusha Jahmiyyah na Ahl-ut-Tamthiyl wanaofananisha Mushabbihah.

Wako kati kwa kati katika mlango wa Matendo ya Allaah (Ta´ala) – baina ya Qadariyyah na Jabriyyah.

Hali kadhalika katika mlango wa Tishio la Allaah – baina ya Murji-ah na Wa´iydiyyah miongoni mwa Qadariyyah na wengineo.

Hali kadhalika katika mlango wa Imani na majina ya Dini – baina ya Haruuriyyah na Mu´tazilah, Murji-ah na Jahmiyyah.

Hali kadhalika kuhusiana na Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – kati ya Rawaafidhw na Khawaarij.

MAELEZO

Mwandishi (Rahimahu Allaah) anasema kuhusu Hadiyth zingine ambazo zimetaja kuhusu sifa ikiwa ni pamoja na Hadiyth ifuatayo:

Dalili ya Sifa mbalimbali za Allaah

“Allaah Ndiye Mola wa mbingu hizi saba na ardhi na Ndiye Mola wa ´Arshi kubwa. Mola Wetu na Mola wa kila kitu. Mpasuaji wa mbegu na kokwa na Ambaye Umeteremsha Tawraat, Injiyl na Qur-aan. Najikinga Kwako na shari ya nafsi yangu na shari ya kila kiumbe kiovu ambacho wewe una utawala juu yake. Wewe ni wa Mwanzo na hakuna kabla Yako kitu. Na Wewe ni wa Mwisho na hakuna baada Yako kitu. Na Wewe ni wa Juu na hakuna juu Yako kitu. Na wewe ni wa Karibu na hakuna kinachojifichika Kwako. Nilipitie deni langu na nitajirishe na ufakiri wangu.”

Katika Hadiyth hii kubwa ambayo ameipokea Muslim ndani yake mna sifa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwamba yuko juu ya ´Arshi, yuko juu ya mbingu, Mola wa ardhi, mteremshaji wa Tawraat, Injiyl na Qur-aan. Zote hizi zinatoa dalili kuonyesha Ujuu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) na kwamba kutoka Kwake ndiko kunateremka kila kitu. Kutoka Kwake kunateremka maamrisho na Wahy ilihali yuko juu ya ´Arshi (Jalla wa ´Alaa). Yuko juu ya viumbe vyote (Subhaanahu wa Ta´ala).

Vilevile mambo yote yako mikononi Mwake na anayaendesha vile anavyotaka (Subhaanahu wa Ta´ala). Yeye ndiye wa Mwanzo na hakuna kabla Yake kitu, wa Mwisho na hakuna kitu baada Yake, wa Juu na hakuna kitu juu Yake na wa Karibu na hakuna kinachofichikana Kwake, kama ilivyokuja katika Qur-aan tukufu:

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

”Yeye Ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho na Aliye juu na Aliye Karibu, Naye kwa kila kitu ni Mjuzi.”(57:03)

Yeye ndiye wa Mwanzo na hakuna kitu kabla Yake, wa Mwisho na hakuna kitu baada yake, Yeye ni wa daima, mkamilifu na hakuacha kutokuwepo (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa msemo mwingine hakuna chochote kilichomtangulia na hafikiwi na kitu kukosekana. Yeye ni wa daima siku zote. Yeye ni wa Juu ambaye yuko juu ya viumbe vyote. Kwa msemo mwingine ni kwamba hakuna kitu kilicho juu Yake. Yeye ndiye wa Juu kabisa, aliye juu ya ´Arshi Yake. ´Arshi ndio sakafu ya viumbe. Yeye ni wa Karibu na hakuna kinachojificha Kwake. Kwa msemo mwingine hakuna Anachohitajia na Yeye anazijua hali za waja Wake na anayajua yaliyomo ndani ya vifua vyao. Katika du´aa hii mna njia ya kuomba kulipiwa deni na kujitosheleza na ufakiri.

Dalili kwamba waumini watamuona Mola wao Aakhirah

Kadhalika kuhusiana na Hadiyth ya Kuonekana:

“Hakika nyinyi mtamuona Mola Wenu siku ya Qiyaamah kama mnavyoona jua wazi wazi pasi na mawingu na kama mnavyouona mwezi usiku wa mwezi mng’aro – hamtosongamana katika kumuona.”[4]

Bi maana mtamuona wazi wazi kabisa. Kuona ni ziada ambayo haihitajii msongamano. Kitu kidogo kuna uwezekano watu wakasongamana na kuambizana wakitazame kwa ajili ya kutoonekana kwake vizuri. Ama kuhusiana na Kuonekana Kwake (Subhaanah) kutakuwa wazi wazi kabisa kama mfano wa linavyoonekana jua pasi na mawingu. Kutakuwa hakuna haja ya kusongamana, kubanana na rabsha. Kila mmoja atamuona akiwa yuko sehemu yake bila ya kupata usumbufu.

Dalili ya Kusikia na Kuona kwa Allaah

Vilevile kuhusiana na Hadiyth pale ambapo walinyanyua sauti zao akawaambia:

“Enyi watu! Zihurumieni nafsi zenu! Kwani hakika hamumuombi ambaye ni kiziwi wala asiyekuwepo.”

Hapa amewabainishia (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) ya kwamba Yeye (Subhaanah) anayasikia maneno na du´aa za waja Wake. Kwa hivyo hahitajii mtu kunyanyua sauti inayopingana na Shari´ah. Kunyanyua sauti kunatakiwa iwe kwa wastani. Kwa ajili hii ndipo akasema kuwaambia:

“Hamumuombi ambaye ni kiziwi wala asiyekuwepo.”

Walikuwa ni wenye kunyanyua sauti zao. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaamrisha wasifanye hivyo ambapo wanapitiliza katika unyanyuaji. Isipokuwa tu wakati wa Talbiyah. Hili ni jambo ambalo limevuliwa. Kuna dalili zenye kuonyesha kuwa inatakiwa kunyanyua sauti. Ama kuhusu kusema “Allaahu Akbar” inatakiwa iwe kwa sauti ya wastani na isiwe kwa kunyanyua sauti sana. Kwani hamumuombi ambaye ni kiziwi wala asiyekuwepo. Yeye yuko juu ya ´Arshi na wakati huo huo yuko pamoja na waja Wake kwa njia ya kwamba anazisikia sauti na maneno yao (Jalla wa ´Alaa). Amesema (Ta´ala):

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ

“Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Aliye karibu – Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba.” (02:186)

Dalili ya Allaah kuwa Karibu na waja Wake

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika yule mnayemwomba Yuko karibu na mmoja wenu kuliko shingo ya mpando wenu.”[5]

Yeye (Subhaanah) yuko karibu na hahitajii mtu akapindukia kwa sauti wakati wa Dhikr. Aombe kwa sauti ya kusikika kidogo kwa njia ya kumdhukuru Allaah na si kwa njia ya kwamba Allaah anahitajia hilo. Anaponyanyua sauti yake kidogo ni kwa njia ya Dhikr na kudhihirisha kumdhukuru Allaah (Jalla wa ´Alaa). Ni kama pale ambapo watu wanapodhihirisha sauti zao wakati wa Talbiyah. Lengo ni kudhihirisha kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall). Vinginevyo ni kwamba Yeye (Subhaanah), ya siri na yaliyojificha, anasikia sauti za waja hata kama watanong´oneza. Hakuna chochote kinachofichikana Kwake. Yeye ni Mwenye kusikia na yukaribu, anazisikia sauti zao hata kama watanong´oneza. Kama ambavyo anazijua hali zao hata kama watazificha. Hakuna chochote kinachojificha Kwake (Jalla wa ´Alaa).

Ni wajibu kwa muumini kumuamini Allaah na kwamba Yeye (Subhaanah) ni Mwenye kusikia na yukaribu, anajua hali za waja Wake, anasikia sauti zao na anajua maombi yao na hakuna chochote chenye kujificha Kwake (Jalla wa ´Alaa) pamoja na kuwa kwa wakati huo huo yuko juu ya ´Arshi na juu ya viumbe wote (Subhaanahu wa Ta´ala). Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ni tofauti na ´Aqiydah ya Ahl-ul-Bid´ah.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, watu wa kati kwa kati

Wako kati kwa kati katika mlango wa Sifa za Allaah… – ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni ´Aqiydah iliyonyooka na ilio kati kwa kati katika mlango huu na mingine. Wako kati kwa kati kuhusiana na Allaah. Kama ambavyo Ummah huu uko kati kwa kati baina ya nyumati zingine basi Ahl-us-Sunnah wako kati kwa kati katika mlango huu pale ambapo wanamthibitishia Allaah sifa na majina Yake pasi na upotoshaji, ukanushaji, kuziwekea namna na kuzilinganisha. Kwa msemo mwingine wanazipitisha kama zilivyokuja na hawazipotoshi, kuzikanusha na kuzilinganisha sifa za Allaah na sifa za viumbe Wake, kama wanavyofanya Jahmiyyah na Mu´tazilah.

Hakika al-Firqat-un-Naajiyah, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, wanaamini hayo… – Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wao wanazithibitisha uthibitisho usiokuwa na ufananishaji na wakati huo huo wanamtakasa Allaah kufanana na viumbe Vyake utakaso usiokuuwa na ukanushaji. Uthibitishaji wa sifa na majina ya Allaah hauhitajii kufananisha kama ambavyo utakaso vilevile hauhitajii ukanushaji. Bali wanasema kuwa wao wanamthibitishia Allaah sifa na majina kwa njia inayolingana Naye pasi na upotoshaji, ukanushaji, kuyawekea namna na kuyafananisha.

Kati ya Jahmiyyah na Mushabbihah

Wako kati kwa kati katika mlango wa Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala)… – Wako kati kwa kati inapokuja katika mlango wa sifa na majina ya Allaah baina ya Ahl-ut-Ta´twiyl ambao ni Jahmiyyah na Ahl-ut-Tashbiyh ambao ni Mushabbihah.

Kuhusu Jahmiyyah wanakanusha sifa na majina ya Allaah. Mushabbihah wao wanayathibitisha, lakini pamoja na hivyo wanasema kuwa Mkono wa Allaah ni kama mkono wangu, Sauti ya Allaah ni kama sauti yangu, Mguu wa Allaah ni kama mguu wangu. Wanafananisha sifa za Allaah na za viumbe. Huu ni uovu mkubwa kabisa. Ni kufuru na upotevu. Wako kati kwa kati baina ya Ahl-ut-Ta´twiyl ambao ni Jahmiyyah na Ahl-ut-Tamthiyl Mushabbihah.

Kati ya Qadariyyah na Jabriyyah

Wako kati kwa kati katika mlango wa Matendo ya Allaah (Ta´ala)…Ahl-us-Sunnah vilevile wako kati kwa kati inapokuja katika mlango wa matendo ya Allaah baina ya Wa´iydiyyah na Qadariyyah. Wanathibitisha matendo ya Allaah na kwamba ni haki. Yeye (Jalla wa ´Alaa) hushuka katika mbingu ya dunia kila usiku, atajionyesha kwa waja Wake siku ya Qiyaamah mpaka waweze kuona uso Wake mtukufu kama unavyoonekana mwezi wazi wazi pasi na kuwepo mawingu (Subhaanahu wa Ta´ala). Huridhia, hughadhibika, huamrisha, hukataza, huumba na huruzuku. Matendo Yake (Subhaanahu wa Ta´ala) ni kitu kimethibiti. Tofauti na Jahmiyyah ambao ni Mu´attwilah na Mu´tazilah wenye kusema kuwa inatakiwa kuthibitisha majina na si sifa. Wanasema kuwa majina ya Allaah yathibitishwe matupu bila ya maana.

Kati ya Murji-ah na Wa´iydiyyah

Hali kadhalika katika mlango wa Tishio la Allaah… – Kadhalika wako kati kwa kati inapokuja katika sifa za Allaah baina ya Wa´iydiyyah ambao wanasema kuwa matishio ya Allaah ni lazima yatekelezwe na Murji-ah wenye kuyaondosha matendo [katika imani] na wanaonelea kuwa mja anachotakiwa ni kutamka na kuamini pasi na kuleta matendo kwa kuwa sio katika imani. Wa´iydiyyah ambao ni Mu´tazilah wao wanategemea makemeo ya Allaah na wasema kuwa mtenda dhambi kubwa atadumishwa Motoni endapo atakufa juu ya maasi. Upande mwingine wa Murji-ah wao wanasema kuwa hakuna kitu chenye kuidhuru imani kwa sababu wanaona kuwa matendo hayaingii katika imani. Wanaonelea mtu akitamka na kusadikisha inatosheleza.

Ahl-us-Sunnah wao wanaonelea kuwa imani ni kutamka, kuleta matendo na kuamini na vilevile maasi yanaidhuru imani. Lakini hata hivyo hayawajibishi kudumishwa Motoni, kama wanavyosema Mu´tazilah. Kadhalika hayamfanyi mtu akakufuru, kama wanavyosema Khawaarij. Lakini maasi yanaidhuru na kuidhoofisha. Kuachana na maasi na kutubu kwayo kunaifanya imani kuwa kamilifu.

Kati ya Haruuriyyah na Mu´tazilah, na Murji-ah na Jahmiyyah

Hali kadhalika katika mlango wa Imani na majina ya Dini… – Aidha Ahl-us-Sunnah wako kati kwa kati baina ya Wa´iydiyyah ikiwa ni pamoja na Mu´tazilah na Khawaarij vilevile na baina Murji-ah. Khawaarij wanasema imani ni kutamka, kufanya matendo na kuamini, lakini haizidi na wala haipungui. Vilevile Wa´iydiyyah wakiwemo Mu´tazilah wanasema kuwa imani ni kutamka, kufanya matendo na kuamini, lakini haizidi na wala haipungui. Mwenye kufa juu ya maasi anakuwa ni miongoni mwa watu wa Motoni na atadumishwa humo milele. Khawaarij wametofautinaa na Mu´tazilah kwa kuona kuwa ni kafiri na wakati huo huo ni katika watu wa Motoni.

Kuhusiana na Ahl-us-Sunnah wao wako kati kwa kati katika hayo. Wanasema kuwa maasi yanaipunguza imani, lakini hayamfanyi mtu akakufuru. Isipokuwa tu pale mtu atapoyahalalisha. Lakini [ikibidi mtu kuingia] hatodumishwa Motoni milele tofauti na wanavyoonelea Khawaarij na Mu´tazilah.

Kati ya Raafidhwah na Khawaarij

Hali kadhalika kuhusiana na Maswahabah wa Mtume… – Ahl-us-Sunnah vilevile wako kati kwa kati inapohusiana na Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baina ya Raafidhwah na Khawaarij. Raafidhwah wamevuka mipaka na Khawaarij wamezembea. Khawaarij wamewapiga vita Maswahabah na wakakufurisha wengi katika wao. Ama Raafidhwah wao wamevuka mipaka kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuhusiana na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wao wanawatakia radhi Maswahabah wote (Radhiya Allaahu ´anhum), wanaamini kuwa wote ni waadilifu na kwamba wao ndio viumbe bora wa Allaah baada ya Mitume (´alayhimus-Swalatu was-Salam). Jengine ni kwamba wanajitenga mbali na mwenendo wa Rawaafidhwah ambao wamepetuka mipaka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na (Radhiya Allaahu ´anhum). Ahl-us-Sunnah hawavuki mipaka na hawazembei. Wao wako upande wa Maswahabah kwa kuwatakia radhi, wanaamini kuwa wao ndio viumbe bora baada ya Mitume na Manabii (´alayhimus-Swalatu was-Salam) na wanaamini kuwa wao ndio viumbe bora kabisa wa Ummah huu. Pamoja na yote haya hawavuki mipaka kwao kama walivyofanya Raafidhwah kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale ambapo wanawaomba pamoja na Allaah na wanadai kuwa wamekingwa na kukosea. Yote haya si sahihi. Raafidhwah wamevuka mipaka na kupotea. Raafidhwah na wao wamezembea inapokuja katika haki ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) na hawakuthibitisha uadilifu wao.

Ahl-us-Sunnah wao wamethibitisha uadilifu wa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) na fadhila zao na kwamba wao ndio viumbe bora baada ya Mitume (´alayhimus-Swalatu was-Salaam). Lakini hata hivyo wameenda kinyume na Raafidhwah katika kuchupa kwao mipaka. Hawakuvuka mipaka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) wala kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Badala yake wanawatakia radhi, wanawaombea msamaha na wanaonelea mwenye kufuata haki miongoni mwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mwema na wanatarajia mema kwake.

[1] Muslim (2713).

[2] al-Bukhaariy (4205) na (6384) na Muslim (2704).

[3] al-Bukhaariy (554) na (574) na Muslim (633).

[4] al-Bukhaariy (4581) na Muslim (183).

[5] al-Bukhaariy (4205) na (6384) na Muslim (2704).

 

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com