34. Si wajibu kulipa swawm ya sunnah

32- Si wajibu kulipa swawm ya sunnah

Si wajibu kwake kulipa siku hiyo. Kuna Hadiyth mbili juu ya hilo:

1- Abu Sa´iyd al-Khudriy amesimulia akisema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitengenezewa chakula ambapo akaja yeye na Maswahabah zake wakanijia. Kilipotengwa chakula kuna mtu mmoja katika kundi lile akasema: “Mimi nimefunga.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ndugu yenu amekualikeni na amejikalifisha kwa ajili yenu.”Fungua na badala yake ufunge siku nyingine – ukitaka kufanya hivo.”[1]

2- Abu Juhayfah amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifunga udugu kati ya Salmaan na Abu Dardaa´. Salmaan akaja kumtembelea Umm Dardaa´ na tahamaki akamkuta katika hali ya kutokuwa na mavazi mazuri. Akasema: “Una nini wewe, ee Umm Dardaa´?” Akajibu: “Ndugu yako, Abu Dardaa´, ni mtu anasimama usiku na mchana anashinda na swawm na hana haja kabisa na dunia. Abu Dardaa´ akaja, akamkaribisha na kumsogezea chakula ambapo Salmaan akawa amemwambia: “Kula!” Akajibu: “Mimi nimefunga.” Akasema: “Ninaapa kwa Allaah ya kwamba endapo hutokula basi na mimi sili.” Akala pamoja naye kisha akalala kwake. Ilipofika usiku Abu Dardaa´ akataka kusimama usiku ambapo Salmaan akamkataza na kumwambia: “Ee Abu Dardaa´! Hakika mwili wako una haki juu yako, Mola wako ana haki, wageni wako wana haki juu yako na mke wako na haki ju yako. Funga wakati fulani na acha kufunga wakati mwingine, swali [usiku] nyakati fulani na mwendee mke wako – mpe kila mwenye haki haki yake. Ilipokaribia kufika asubuhi akamwabia: “Inuka sasa [na uswali] ukitaka ambapo akawa amesimama, wakatawadha kisha wakatoka kwenda kuswali. Abu Dardaa´ akasogea karibu na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili amweleze yale aliyomwambia Salmaan. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Ee Abu Dardaa´! Hakika mwili wako una haki… kama alivyomwambia Salmaan!”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Amesema kweli Salmaan.”[2]

[1] Ameipokea al-Bayhaqiy (04/279) kwa mlolongo wa wapokezi mzuri, kama alivyosema al-Haafidhw katika “al-Fath” (04/170). Ameipokea vilevile at-Twabaraaniy katika “al-Awsatw” (01/132/01). Nimeipokea vilevile katika “al-Irwaa´” (1952) upokeaji ambao unatilia nguvu kuthibiti kwake.

[2] Ameipokea al-Bukhaariy (04/170-171), at-Tirmidhiy (03/290), al-Bayhaqiy (04/276) na siyaaq ni yake. at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 159-161
  • Imechapishwa: 24/03/2018