34. Mume anatakiwa ayashinde mapenzi ya mke

Miongoni mwa haki za mke juu ya mume ni yeye ayashinde mapenzi yake kwa maneno na hali hata kama atapetuka mipaka, kumsifu kwa asokuwa nayo au akamueleza jinsi anavyompenda na wakati ndani ya moyo ni kidogo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemruhusu mume kumdanganya mke wake na kinyume chake. Ni sawa mume akamdanganya mke wake ili awe na furaha nyumbani. Amtajie uzuri wake kwa njia asokuwa nayo. Amweleze kuwa anampenda kwa njia asiyoihisi moyoni mwake. Akimuomba kitu asichoweza kukileta na anachelea lau atasema kuwa hatomletea atamkasirikisha na kufanya maisha kuwa kama moto, anaweza kusema kuwa atamletea na kisha baadae akasema kuwa hakukipata au kwamba kina bei kubwa kwa sasa. Uongo kama huu ni mzuri ikiwa kama unachangia kuleta furaha kwa wanandoa.

Mwanaume mwema anampambia mke wake kwa njia inayoendana na wanaume kwa aina ya manukato na muonekano mzuri. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ

Na hao wanawake wana kama ile [haki juu ya mume] iliyo juu yao kwa wema.”[1]

Mfasiri wa Qur-aan Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mimi nampambia mwanamke kama jinsi ninavyotaka anipambie.”

Njia nyingine ya kushinda mapenzi ya mke wake ni yeye kumsaidia kazi za nyumbani. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye alikuwa ni Nabii wa Allaah na Mtume anayeteremshiwa Wahyi kutoka Kwake, alikuwa akisaidia kazi za nyumbani na wakati kunapoadhiniwa anatoka na kwenda kuswali[2].

Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwatendea wake zake wema na kheri. Alikuwa akitania nao na mpole kwao. Baada ya kuwa ameshafikisha umri wa miaka khamsini na tatu alifanya mashindishano ya mbio na ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa). ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza jinsi alivokuwa bado ni msichana mdogo na alikuwa katika safari pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaambia Maswahabah zake watangulia mbele, na wakafanya hivo. Baada ya hapo akasema kumwambia:

“Hebu njoo tushindishane.”

Amesema:

“Nikakimbia naye na kumshinda.”

Tazama Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivokuwa akiishi! ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Akanyamaza. Baada ya kuongezeka uzito na kusahau tukio hilo nilikuwa pamoja naye katika safari. Akawaambia Maswahabah zake watangulie mbele, wakafanya hivo. Kisha akasema: “Hebu njoo tushindishane.” Nikasema: “Vipi nitashindishana na wewe ilihali niko katika hali kama hii?” Akasema: “Ni lazima ufanye.” Nikaanza kukimbia naye na akanishinda. Akaanza kucheka na kusema: “Hili ni lipizo la wakati ule.”[3]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alikuwa ameshasahau tukio hili, lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa bado hajasahau. Alikuwa akitania na wake zake, akijipendekeza kwao na kushindana nao. Ni jambo lenye dhana ya nguvu ya kwamba hili lilikuwa mwishoni wa maisha yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Miongoni mwa kuishi kwake vizuri (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni pamoja na ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) siku moja alisema:

“Ee kichwa changu!” Mtume wa Allaah akawa amesema: “Hapana, bali mimi ee kichwa changu!”[4]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Nilikuwa nala nyama ilihali niko na hedhi. Halafu nikaimpa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akaitia mdomoni mwake mahala pale pale ambapo mimi niliweka. Kisha nanywa na kumpa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akanywa na kuweka mdomo wake mahala pale pale ambapo mimi niliweka mdomo wangu.”[5]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiweka kichwa chake kwenye mapaja yangu na kusoma wakati ambapo nilikuwa na hedhi.”[6]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akilala usiku na mke wake kwenye shuka moja hata kama alikuwa na hedhi. Akipatwa na kitu katika damu yake, hupaosha[7]. Vilevile Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akioga na mke wake kwenye chombo kimoja[8].

Huku ndio kuishi kwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yeye alikuwa ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwetu ana kiigizo chema. Huenda baadhi ya waume wakasema kuwa wameshakuwa wazee na wameshachelewa kwa sasa na kwa hivyo hawana haja ya kufanya haya. Lakini huyu hapa [mtazame] Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na mizigo isiyoweza kubeba mamilioni ya wanaume. Amebeba matatizo ya Ummah, amebeba ujumbe na amefikisha umri mkubwa. Pamoja na hayo yote anashindana na mke wake na anasubiri tu fursa nzuri ya kufanya hivo. Ni uzuri uliyoje mume akamchukua mke wake kumpeleka sehemu na kutaniana naye, akashindana naye na akamfanya afurahi!

[1] 2:228

[2] Ibn Abiy Shaybah (5/272), Ibn Abiy Haatim (2/2196), at-Twabariy (4/4768) na al-Bayhaqiy (7/295).

[3] Ibn Hibbaan (10/4691), an-Nasaaiy (5/8942), Ahmad (6/39), al-Humaydiy (1/128/261) na at-Twahaawiy (5/143). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (131).

[4] al-Bukhaariy (5666).

[5] Muslim (300), Abu Daawuud na wengine.

[6] al-Bukhaariy (297), Muslim (301) na Abu Daawuud (260).

[7] Abu Daawuud (269), an-Nasaaiy (284), Ahmad (6/45) na wengine kupitia ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

”Mimi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tulikuwa tukilala kwenye shuka moja na wakati nina hedhi. Akipatwa na kitu huosha mahala hapo na si zaidi ya hivo. Kisha huswali nayo. Na nguo yake ikipatwa na kitu huosha mahala hapo na si zaidi ya hivo. Kisha huswali nayo.”

Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (269).

[8] al-Bukhaariy (273) kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

”Mimi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tulikuwa tukioga kwenye chombo kimoja na tukipasiana maji.”

Tazama Muslim (321).

 

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 24/03/2017