34. Mikono miwili ya Allaah yote ni ya kuume

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

“Mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kulia.” (39:67)

Katika Hadiyth kumetajwa mkono wa kulia na wa kushoto yote miwili. Lakini hata hivo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mikono Yake yote ni ya kuume.”[1]

Ni mkono wa kushoto ukiwa na maana ya wa kuume. Hilo ni kutokana na kumtakasa Allaah (´Azza wa Jall) kutokamana na mapungufu. Kwa kuwa huenda akisikia mwenye kusikia kuhusu Allaah kuthibitishiwa mkono wa kushoto, huenda akaingiwa akilini mwake kwamba ni kama mfano wa mkono wa kushoto wa kiumbe. Kwa sababu mkono wa kushoto wa kiumbe sio kama mkono wa kulia. Mkono wake wa kushoto una kasoro. Jengine kama mnavojua ni kuwa mkono wa kushoto ni wenye kuondosha taka na kujisafisha. Kuhusu mkono wa kuume ni bora zaidi na ndio mkono wenye kupokea na kupeana kitu, kula, kunywa na mengineyo. Hivyo akisikia mwenye kusikia kuwa Allaah anathibitishiwa mkono wa kushoto, huenda akaingiwa moyoni mwake kwamba na wenyewe ni mpungufu kuliko mkono wa kuume, kama ilivyo kwa viumbe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakanusha mawazo haya na akasema:

“Mikono Yake yote ni ya kuume.”

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“Na mikono Yake yote miwili.”

Bi maana mikono ya Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… kwa fadhilah…”

Bi maana kwa kutoa na kutunuku.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“… ni yenye kutoa.”

Bi maana inatoa kuwapa na kuwatunuku viumbe. Imekuja katika Hadiyth:

“Mikono Yake imejaa inatoa usiku na mchana. Hivi huoni Alivyotoa tangu alipoumba mbingu na ardhi. Hakika havijapungua vilivyomo kwenye mkono Wake wa kuume.”

Hakika Yeye (Jalla wa ´Alaa) anatoa vya kutoa pasi na mpaka wala kikomo. Anatoa kwa mkono Wake mtukufu kuwapa waja Wake.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“Na mikono Yake yote miwili kwa fadhilah ni yenye kutoa.”

Bi maana kwa kutoa na kwa fadhila za Allaah.

“… ni yenye kutoa.”

Bi maana ni yenye kuendelea kutoa pasi na kusitisha (Subhaanahu wa Ta´ala).

Mayahudi – Allaah awakebehi – pindi walipomsifu Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa ubakhili wakasema:

يَدُ اللَّـهِ مَغْلُولَةٌ

“Mkono wa Allaah umefumbwa.”

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akasema:

غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا بِمَا قَالُوا ۘ بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَاءُ

“Bali mikono Yake imefumbuliwa hutoa Atakavyo.” (05:64)

Bi maana imefumbuliwa kwa ukarimu na kwa kutoa.

[1] Muslim (18) na (1827)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 93-95
  • Imechapishwa: 09/01/2024