34. Jahmiyyah wamejifananisha na makafiri katika masuala ya Qur-aan


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Naamini kuwa Allaah ni Mwenye kufanya Akitakacho na hakukuwi kitu isipokuwa kwa kutaka Kwake, hakitoki kitu nje ya utashi Wake, hakuna kitu ulimwenguni kinachotoka nje ya makadirio Yake na wala hakitoki isipokuwa kutokana na makadirio Yake.

MAELEZO

Shaykh (Rahimahu Allaah) ameyamaliza masuala ya maneno ya Allaah na amekwishabainisha ´Aqiydah yake juu ya jambo hilo, kwamba ni ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na kwamba ni mwenye kujiweka mbali na ´Aqiydah ya Jahmiyyah, Mu´tazilah na Ashaa´irah ambao wameyaingilia maneno ya Allaah na wakasema maneno mabaya na wengine wakasema maneno ya makafiri waliosema kuwa Muhammad ndiye anayezua Qur-aan hii na akaja nayo na kumnasibishia nayo Allaah (´Azza wa Jall). Haya ni maneno ya makafiri. Kwa ajili hii al-Waliyd bin al-Mughiyrah alisema kuwa Qur-aan si jengine isipokuwa ni maneno ya mtu[1]. Amesema (Ta´ala) akielezea juu yake:

إِنَّهُ فَكَّرَ وَقَدَّرَ فَقُتِلَ كَيْفَ قَدَّرَ ثُمَّ قُتِلَ كَيْفَ قَدَّرَ ثُمَّ نَظَرَ ثُمَّ عَبَسَ وَبَسَرَ ثُمَّ أَدْبَرَ وَاسْتَكْبَرَ فَقَالَ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ يُؤْثَرُ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ

“Hakika yeye alitafakari na akakadiria, basi alaaniwe namna alivyokadiria, kisha alaaniwe namna alivyokadiria, kisha akatazama, kisha akakunja kipaji na akanuna, kisha akageuka nyuma na akafanya kiburi. Akasema: “Hii si chochote isipokuwa ni uchawi unayonukuliwa.  Hii si chochote isipokuwa ni kauli ya mtu.”[2]

Bi maana kwamba Qur-aan ni maneno ya Muhammad na kwamba haikusemwa na Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Jahmiyyah wakajifananisha na makafiri katika suala hili na wakasema kwamba Qur-aan sio maneno ya Allaah na kwamba ni maneno ya Muhammad.

[1] Tazama ”Tafsiyr Ibn Kathiyr” (04/443).

[2] 74:18-25

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 55
  • Imechapishwa: 17/03/2021