214- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau dunia hii mbele ya Allaah ingelikuwa sawa na ubawa wa nzi basi kafiri asingekunywa kikombe cha maji.”[1]

215- Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita katika soko kutoka kwa juu. Watu wakamzunguka. Akapita karibu na kuku aliyekufa mwenye masiko madogo. Akayashika masikio yake na kusema: “Mnaitaka?” Wakasema: “Lau ingekukuwa bado iko hai basi ingelikuwa ni yenye mapungufu kwa sababu ya masikio yake madogo, sembuse hivi imeshakufa.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ninaapa kwa Allaah ya kwamba Allaah ni mwenye kuidharau dunia hii kuliko nyinyi mnavyoidharau hii.”[2]

216- Wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah) wamesema:

“Allaah kuidharau dunia hii ina maana ya kwamba hakuiumba na kufanya ndio malengo, bali Ameifanya ni njia yenye kupelekea katika lengo lingine. Dunia hii Hakuifanya ni mahali pa kudumu. Dunia hii Hakuifanya ni mahali pa malipo. Dunia hii ni safari na majaribio. Mara nyingi Huwafanya makafiri na wajinga wakaburudika nayo na Akawalinda nayo Mitume na mawalii. Kunakutosheleza kuona uduni wake kutambua kuwa Allaah anaiona ndogo, anaidharau, anailaumu na anaichukia na watu wake wenye kuipenda. Hayuko radhi isipokuwa na mwerevu mwenye kuipa nyongo na kujiandaa na safari iliyoko mbele. Pamoja na uduni wake ni lazima kwa mtu kueshi kwayo kwa sababu ndio njia yenye kukusudiwa na njia yenye kusifiwa.”

217- Kuna mtu aliilaumu dunia hii mbele ya ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh). ´Aliy akasema:

“Dunia hii ni nyumba ya ukweli kwa yule ambaye ni mkweli ndani yake, nyumba ya uokozi kwa yule mwenye kuifahamu na nyumba ya utajiri kwa yule mwenye kukusanya ndani yake.”

218- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Dunia ni yenye kulaaniwa na vilivyomo ndani yake ni vyenye kulaaniwa isipokuwa kumdhukuru Allaah na vyote vilivyo na maana yake, mwanachuoni na mwanafunzi.”[3]

219- ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Dunia italetwa mbele ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ambapo Mola (Tabaarak wa Ta´ala) atasema: “Chukua vile vilivyo vyetu na vilivyobaki vitupe Motoni.”[4]

[1] at-Tirmidhiy (2422).

[2] Muslim (18/93).

[3] at-Tirmidhiy (2424) ambaye amesema kuwa ni nzuri na geni na Ibn Maajah (4122).

[4] Dhamm-ud-Dunyaa (6) ya Ibn Abiyd-Dunyaa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 126-128
  • Imechapishwa: 18/03/2017