Ndugu wapendwa! Tumekwishazungumza kuhusu mafungu matano ya watu juu ya hukumu ya kufunga. Hii leo katika kikao hichi tutazungumza kuhusu fungu la sita katika mafungu hayo:

6- Msafiri ikiwa hakukusudia kwa safari yake kufanya ujanja ili asipate kufunga. Akikusudia kufanya hivo basi hapo kufungua juu yake itakuwa ni haramu na kufunga itakuwa ni lazima. Asipokusudia kufanya hila basi ni mwenye khiyari kati ya kufunga na kutofunga. Ni mamoja muda wa safari yake utarefuka au utafupika. Ni mamoja vilevile safari yake imezuka kwa sababu fulani au ni yenye kuendelea. Kama mfano wa rubani au dereva wa teksi. Hilo ni kutokana na ujumla wa maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

”Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo. Allaah Anakutakieni mepesi.”[1]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kwa kusema:

“Tulikuwa tukisafiri pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aliyefunga hakumtia dosari ambaye hakufunga wala ambaye hakufunga hakumtia dosari mwenye kufunga.”

Muslim amepotea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Walikuwa wanaona yule mwenye kupata nguvu akafunga kitendo hicho ndio bora zaidi. Na walikuwa wanaona yule mwenye kuhisi unyonge ambapo akala kitendo hicho ndio bora zaidi.”

Abu Daawuud amepokea katika “as-Sunan” yake kupitia kwa Hamzah bin ´Amr al-Aslamiy ambaye alisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Mimi ni mgonjwa mgongoni na pengine mwezi huu ukanikuta – bi maana Ramadhaan – na mimi nahisi nguvu na ni kijana. Ee Mtume wa Allaah! Naona kuwa kufunga ndio kwepesi zaidi kwangu kuliko kuchelewesha na hivyo ikawa ni deni kwangu.  Ee Mtume wa Allaah! Nikifunga ndio ujira mkubwa zaidi au nile?” Akasema: “Ee Hamzah! Chochote katika hayo utachopenda.”[2]

Ikiwa dereva wa teksi kufunga katika Ramadhaan ni kugumu kwake, kwa mfano kutokana na joto kali, basi ataichelewesha mpaka katika wakati ambapo hali ya hewa ni yenye baridi na itakuwa ni wepesi kwake kufunga.

[1] 02:185

[2] Katika cheni ya wapokezi wake kuna unyonge. Lakini ina shawahidi na asili yake iko katika ”as-Swahiyh” ya Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 46-51
  • Imechapishwa: 25/04/2020