34. Du´aa ya Mtume kabla ya vita vya Badr

Mapambano yakawa mapambano kwelikweli na nusura ikateremshwa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akajitahidi na akaomba du´aa kwelikweli mpaka nguo yake ya juu ikawa inamshuka kutoka mabegani mwake. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) akawa anaipandisha na kusema:

“Ee Mtume wa Allaah! Usijichoshe kumuomba Mola wako sana kiasi hivo. Hakika atakutimizia ahadi Aliyokupa.”

Na huku Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Ee Allaah! Kikiangamia kikundi hichi basi hutoabudiwa ardhini.”

Hapo ndipo Allaah (Ta´ala) akateremsha:

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ

“Wakati mlipomuomba uokovu Mola wenu Naye akakuitikieni kwamba: “Hakika Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu wafuatanao mfululizo.”[1]

Kisha akasinzia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya muda kidogo akainua kichwa chake na kusema:

“Pata bishara njema ee Abu Bakr! Huyu hapa Jibriyl akiwa na udongo kwenye meno yake ya mbele.”[2]

[1] 08:09

[2] al-Bayhaqiy katika ”Dalaa-il-un-Nubuwwah” (3/81).

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 50-51
  • Imechapishwa: 09/10/2018